CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA –ZNZ) kinaiasa jamii kujizuia kurikodi watoto wadogo na kuwaweka katika mitandao baada ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji kwani kufanya hivyo ni kuwadhalilisha zaidi.
Kufuatia kuenea kwa simu janja/mtetemo kumeibuka watu ambao wanarikodi watoto na kusambaza taarifa zao kupitia picha, sauti na video kinyume na taratibu na maadili ya uandishi wa habari.
Tunaamini kwamba watu hawa wana nia njema ya kutaka haki itendeke na kuwatia ujasiri zaidi watoto lakini tunashauri wasifanye kazi hiyo na badala yake wawaaachie waandishi wa habari ambao wamesomea kazi hiyo na hivyo wanajua kuficha utambulisho wa watoto hao.
Watoto wana haki ya kulindwa dhidi ya vitendo vyote vya udhalilishaji, vitisho vya usalama wao na unyanyasaji wa mtandaoni, sambamba na kulinda taarifa zao binafsi.
Sheria ya Mtoto Na. 6, 2011 kifungu cha 33 (1) kinakataza mtu yoyote kutoa taarifa au kuchapisha picha ambayo itapelekea kumtambulisha mtoto aliyeathirika bila ya amri ya Mahakama.
Tunaiomba pia Serikali kwa kushirikiana na wadau kuandaa mkakati imara utakaosaidia kutoa elimu hii kwa wana jamii ili kuzuia vitendo hivi vya kurikodi na kusambaza taarifa za watoto.
Kwa mujibu wa uhakiki wa habari uliofanywa na TAMWA Zanzibar hivi karibuni ni kuwa waandishi wa habari wanaelewa umuhimu wa kumlinda mtoto dhidi ya mitandao na kwamba habari zao huficha taarifa za wahanga, hivyo video zinazofichua taarifa za watoto huwa mara nyingi zinatoka kwa watu wasio na taaluma ya uandishi wa habari.
Tukio la hivi karibuni linahusisha mtoto mdogo anayedaiwa kubakwa na baba yake mlezi ambaye bado hajatiwa hatiani na vyombo vya sheria na hivyo TAMWA,ZNZ inaiomba Serikali na vyombo husika kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa pindi ikibainika ukweli wake ili iwe ni funzo kwa wazee wengine wenye tabia kama hizo.
Watoto wamekuwa ni wahanga wakubwa wa kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji ambavyo vinawaathiri kimwili, kisaikolojia na hata katika maendeleo yao kwa ujumla na malalamiko yapo kwenye utoaji wa hukumu bado ni mdogo. Kwa mujibu wa taarifa ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali matukio 1360 ya udhalilishaji yaliripotiwa mwaka 2022 na kwamba ni matukio 181 tu sawa na asilimia 13 ndiyo yaliyotiwa hatiani