Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Shaaban Ramadhan Abdalla akizungumza na wasaidizi wa kisheria wakati akizindua Jukwaa la tatu la mwaka la msaada wa Kisheria lililofanyika Chuo cha Utalii Maruhubi.
Mkurugenzi Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Hanifa Ramadhani Said akitoa maelezo mafupi kuhusiana na Jukwaa la 3 la msaada wa kisheria lilofanyika Chuo Cha Utalii Maruhubi .
Mwakilishi wa Taasisi ya LFS, Wakili Alphonce Gura akitoa salamu za Taasisi katika Jukwaa la tatu la mwaka la msaada wa kisheria lililofanyika Chuo cha Utalii Maruhubi.
Mwakilishi kutoka wizara ya Katiba na sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Edith Shekidele akizungumza katika Jukwaa la tatu la mwaka la msaada wa Kisheria lililofanyika Chuo cha Utalii Maruhubi.
Katibu Mkuuu OR-KSUUB Mansura M .Kassim akizungumza machache na kumkaribisha Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Shaaban Ramadhan Abdalla kufungua Jukwaa la 3 la msaada wa kisheria lilofanyika Chuo Cha Utalii Maruhubi .
Mkuu wa Skuli ya Sheria Dkt.Ali Uki akiwasilisha mada katika Jukwaa la tatu la mwaka la msaada wa Kisheria lililofanyika Chuo cha Utalii Maruhubi.
Mkurugenzi Idara ya uratibu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Zainab Khamis Kibwana wapili kulia akichangia mada katika Jukwaa la tatu la mwaka la msaada wa Kisheria lililofanyika Chuo cha Utalii Maruhubi.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MALEZO
Na Fauzia Mussa-Maelezo
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt.Mwinyi Talib Haji amewaomba watoa huduma za msaada wa kisheria kuendeleza jukumu hilo kwa maslahi ya Nchi.
Akizungumza wakati akifungua Jukwaa la tatu la Msaada wa Kisheria kwa niaba ya Mkuu huyo Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Shaaban Ramadhan Abdalla alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua na kuthamini mchango wa wadau hao katika kuhakikisha jamii isiyo na uwezo inafikiwa vilivyo na kupata haki zao.
Alisema watoa huduma hizo wamekuwa wakifikisha huduma za msaada wa kisheria ngazi ya jamii, hivyo aliwataka kulitumia Jukwaa hilo katika kujadili , kubadilishana uzowefu, kuimarisha mashirikiano juu ya maswala ya msaada wa kisheria na kuendeleza juhudi za Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa haki za jamii ya Wazanzibar.
Aidha, aliwataka washiriki hao kuwa watulivu katika Jukwaa hilo pamoja na kuitumia kauli mbiu ya mwaka huu kuwa chachu ya mabadiliko ya utendaji kazi na kuja na mikakati mipya ya kuendeleza utoaji wa huduma za msaada wa kisheria zilizobora na zenye kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Dkt. Mwinyi Talib alifurahishwa na utekelezwaji wa maazimio yaliofikiwa na Idara ya katiba na msaada wa kisheria kupitia utekelezaji wa Jukwaa la pili la msaada wa kisheria na kuwataka katika Jukwaa la tatu kuondoka na maazimio yatakayoimarisha maswala ya kisheria hasa katika mwelekeo wa mapitio ya Sera ya msaada wa kisheria ya mwaka 2017 na kupelekea mabadiliko ya sheria ya msaada wa kisheria No.13 ya mwaka 2018.
Hatahivyo aliwashauri watendaji wa Idara ya Katiba na msaada wa kisheria katika majukwaa yajayo kushirikisha watoa msaada wa kisheria kutoka nje ya Tanzania ili kupata uzowefu zaidi.
Awali alilishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP na Taasisi ya LSF kwa juhudi zao za kuunga mkono watoa huduma za msaada wa kisheria na kuendeleza ufadhili wao katika miradi mbalimbali Nchini.
Akizungumzia kuhusu Jukwaa hilo Mkurugenzi Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Hanifa Ramadhani Said alisema lengo kuu la kufanyika kwa Jukwaa hilo ni kukuza ubunifu, kuimarisha ufanisi na uweledi wa utendaji wa majukumu kwa watoaji wa msaada wa kisheria na kuwezesha upatikananji wa Sera mpya zinazokidhi mahitaji ya jamii katika upatikanaji wa huduma za kisheria pamoja na kuwaunganisha watoaji wa msaada wa kisheria na taasisi nyengine ili kuwawezesha kufanya kazi kwa pamoja .
Alifahamisha kuwa katika Jukwaa hilo mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo mada ya utekelezaji wa Sera na Sheria ya msaada wa kisheria kwa lengo la kupeleka mbele harakati za msaada wa kisheria.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Taasisi ya LFS, Wakili Alphonce Gura, alisema kwa sasa Zanzibar imekuwa sehemu ya kujifunzia katika utoaji wa msaada wa kisheria kwa Nchi za Afrika Mashariki hivyo taasisi hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada hizo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kongamano hilo la siku mbili liliwashirikisha watoa huduma za msaada wa kisheria kutoka Zanzibar na Tanzania Bara ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “kuimarisha huduma za msaada wa Kisheria zenye ubora na zinazozingatia matokeo”