Na. Damian Kunambi, Njombe
Wakazi wa vijiji vinne vya Tarafa ya Masasi wilayani Ludewa mkoani Njombe vinaenda kuondokana na changamoto ya kuhatarisha maisha yao kwa kuliwa na Mamba pindi waendapo kuchota maji katika mto Ruhuhu baada ya serikali kupeleka mitambo ambayo tayari imekwisha anza kuwachimbia visima na vitakavyo wapatia maji safi na salama.
Hatua hiyo imefikiwa mara baada ya wananchi hao kufikisha kilio chao kupitia vyombo vya habari pamoja na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga ambaye hivi karibuni alishindwa kuendelea na mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kiyogo kilichopo katika kata ya Masasi kutokana na wananchi hao kuimba nyimbo za huzuni juu ya kukosa huduma ya maji huku wakibubujikwa na machozi kitu ambacho kilimlazimu mbunge huyo kuahirisha mkutano na kuahidi kurejea tena pindi atakapopata maji hatimaye mbunge huyo amerejea tena kufanya mkutano huo akiwa na mitambo ya kuchimba visima hivyo.
Akizungumza mbele ya mkutano wa wananchi wa kijiji hicho Meneja wa Mamlaka ya maji Mijini na Vijijini (RUWASA) Eng. Jeremiah Maduhu amesema visima hivyo vitachimbwa katika kijiji cha Kiyogo kata ya Masasi, na katika kata ya Manda vitachimbwa katika kijiji cha Nsungu, Igalu na kijiji cha Mbongo kwa urefu wa mita 150 kwenda chini.
” Mheshimiwa mbunge siku chache zilizopita uliahirisha mkutano wako ukasema unaenda kutafuta maji, naomba nikupongeze wewe na Rais wetu kwa kuhakikisha mitambo hii inaletwa katika kijiji hiki cha Kiyogo na kutatua changamoto hii kwani mradi huu ilitakiwa ukamilike muda mrefu kwa kupitia mradi wa Lifua lakini kwa bahati mbaya mradi huo haukuweza kutoa maji ya kutosha kusambaza na maeneo mengine.
Mesema mitambo hiyo haitatoka katika kijiji hicho mpaka wahakikishe maji yamepatikana na tayari wamekwisha andaa tenki la lita elfu 25, vituo vya kuchotea maji 6,wamesha chimba mitaro kwaajili ya kulaza mabomba hayo hivyo wananchi wa kijiji hicho muda si mrefu watapata maji safi na salama.
Hata hivyo wananchi wamefurahishwa na hatua hiyo iliyofikiwa akiwemo Eater Makunguru akisema kuwa imewalazimu kuweka uzio katika mto huo huku wakisindikizina watu zaidi ya watano lakini pamoja na kufanya hivyo bado imekuwa changamoto kwani Mamba bado wanawavizia na kuwakamata.
” Hujio wa hii mitambo ni matumaini tosha kwamba tayati tumeshapata maji, tunamshukuru sana Rais wetu pamoja na Mbunge kwani wameleta furaha katika kijiji chetu na kutuondosha katika ile Jehanam” amesema Bi. Makunguru.
Aidha kwa upande wake mbunge wa jimbo la Ludewa joseph kamonga amesema Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mama mwenye huruma kwani kwa muda mfupi tuu tangu wananchi hao wapaze sauti zao ameweza kutatua changamoto hiyo.
“Rais amekuwa akigawa rasilimali za nchi kwa usawa kwa kila wilaya na mambo mengine amekuwa aliyafanya kimya kimya pasipo kuzungumza” amesema Kamonga.
Ameongeza kuwa katika mradi wa Lifua ambao umeonekana kuwa na changamoto katika kuwafikia wananchi wengi tayari Rais ametaka liandikwe andiko ili kuuboresha na yuko tayari kutoa fedha za uboreshaji huo mara tuu andiko hilo litakapo kamilika.