Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb), akikagua uendelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja B kinachojengwa katika eneo la Mtuzu Kata ya Butiama Wilayani Butiama Mkoani Mara leo Novemba 18, 2023.
Muonekano wa Jengo la Kituo cha Polisi Daraja B kinachojengwa katika eneo la Mtuzu Kata ya Butiama Wilayani Butiama Mkoani Mara Novemba 18, 2023.
Na Mwandishi Wetu;
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama Mhe. Jumanne Sagini ameagiza kukamilika kwa wakati Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja B cha Wilaya ya Butiama Mkoani Mara, ifikapo mwezi Disemba 2023 kama ilivyoelekezwa.
Maagizo hayo ameyatoa leo Novemba 18, 2023 wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua uendelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo hicho kilichopo katika eneo la Mtuzu Kata ya Butiama Wilayani Butiama.
“Nimefurahishwa na kasi ya Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Butiama, mradi huu unatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu mpendwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, bila kuchoka mama huyu amemwaga fedha za kutosha hivyo basi nimtake mkandarasi kukamilisha mradi haraka bila vikwazo kwani Wananchi wana kiu kubwa ya kupata huduma karibu,” Alisema
Katika taarifa yake Meneja wa Mradi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Butiama wa Kikosi cha Polisi Ujenzi, Mkandarasi SP Masiva Mfinanga alieeleza kuwa, mradi huo una thamani ya Shilingi Milioni 802,000,000.00 ambapo ujenzi ulianza rasmi Mei 6, 2023 na unategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Disemba 2023.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama Mhe. Jumanne Sagini yupo Mkoani Mara kwa ziara yake ya kikazi ambapo atatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi inayoendelea katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo chini ya Wizara hiyo.