Nyumba ya mitambo ya kusukuma maji iliyojengwa kupitia mradi wa maji wa Mahenje wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbozi Mhandisi Ismail Nassor kushoto,akielezaa juu ya kukamilika kwa mradi wa maji Mahenje kata ya Mahenje wilayani humo,wa pili kushoto mganga wa zahanati ya Myovizi Esperata Simbila,kulia Diwani wa kata ya Mahenje Japhet Mganga na wa pili kulia katibu wa Chombo cha watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO) Prakseda Mireni.
Na Muhidin Amri,Mbozi
JUMLA ya vijiji vinane vya wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe,vinatarajia kuondokana na adha ya maji safi na salama baada ya Serikali kutenga zaidi ya Sh.bilioni 11 kwa ajili ya ujenzi wa miradi mipya 7 ya maji.
Kati ya fedha hizo, Sh.bilioni 8 zinatokana na mpango wa lipa kwa matokeo(P4R) na Sh.bilioni 3 za mfuko maji.
Vijiji hivyo ni Isansa,Mbozi mission,Ikonya,Makolo,Chimbuya,Bara,Ilomba Idiwili na kijiji cha Lungwa ambavyo tangu vilipoanzishwa havijawahi kupata maji ya bomba hivyo wananchi wanaendelea kutumia maji ya visima vya asili na mito.
Hayo yamesemwa jana na Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbozi Ismail Nassor,wakati akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa huduma ya maji na ujenzi wa miradi mpiya ya maji inayokwenda kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Alisema,kukamilika kwa miradi hiyo kutawezesha wananchi wa vijiji hivyo kupata maji ya uhakika,kuchochea shughuli za maendeleo na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 75 ya sasa hadi asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.
Aidha Ismail alisema kuwa,kwa sasa Ruwasa inaendelea kukamilisha miradi 9 ambayo ilianza kutekelezwa mwaka uliopita na iko hatua mbalimbali za utekelezaji na inakamilika mwezi Disemba mwaka huu.
Pia alisema,kabla ya Ruwasa haijaanza kazi mwaka 2019 hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo ilikuwa asilimia 35,lakini kwa muda wa miaka mitatu wamefanikiwa kujenga jumla ya miradi 27 iliyowezesha huduma ya maji kuongezeka hadi kufikia asilimia 75 mwaka 2023.
Kwa mujibu wa Ismail,baadhi ya miradi iliyojengwa na kukamilika ni mradi wa maji Mahenje unaohudumia zaidi ya watu 12,000 wa kijiji hicho uliotekelezwa kwa fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uvico-19 kiasi cha Sh.milioni 397.
Alisema,kabla ya mradi huo wananchi walitumia maji ya visima na madimbwi ambayo hayakuwa safi na salama,hivyo kusababisha baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mahenje kupata magonjwa ya matumbo na magonjwa ya mlipuko mara kwa mara ikiwemo kuharisha.
Diwani wa kata ya Mahenje Japhet Ntandala,ameishukuru serikali kukamilisha mradi huo kwani umesaidia kumtua mama ndoo kichwani na kuwaondolea adha wananchi wa kijiji hicho kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwa matumizi yao.
Hata hivyo,ameiomba wakala wa maji na usafi wa mazingira(Ruwasa)kupeleka mtandao wa maji ya bomba kwenye vijiji viwili vilivyobaki ambavyo havina maji safi na salama.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa zahanati ya Mahenje Dkt Esperata Simbila alisema,mradi huo umesaidia sana kupunguza magonjwa ya kuambukizwa kama vile kipindupindu na ugonjwa wa matumbo.
Ameitaka jamii, kuhakikisha inatumia maji ya bomba ambayo ni safi na salama kwa ajili ya kulinda afya zao badala ya kutumia maji ya visima vya asili ambayo siyo salama.
Mhasibu wa chombo cha watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO)Prakisda Mireni alisema,hadi sasa jumla ya kaya 62 zimeshavuta maji majumbani na kuna maombi zaidi ya 100 ya watu wanaohitaji kuingiza maji kwenye nyumba zao.