Na Veronica Simba, LINDI
Jumla ya vijiji 455 kati ya 524 vya Mkoa wa Lindi vimekwishafikishiwa huduma ya umeme na kazi inaendelea katika vijiji 69 vilivyosalia, ambapo hadi kufikia Desemba 30 mwaka huu, vyote vitakuwa vimefikiwa.
Hayo yamebainishwa Novemba 17, 2023 wakati wa ziara ya Viongozi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu.
Akitoa takwimu, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu amesema “katika Mkoa wa Lindi, Serikali imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 116 kwa ajili ya kazi za umeme vijijini.
Akizungumza na Ujumbe huo wa Viongozi ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack amekiri kuwa umeme vijijini umebadilisha kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi.
“Vile vitu ambavyo vilikuwa mijini tu, sasa viko vijijini. Watu wamepata umeme na wameweza kufanya vitu vingi. Friji ziko vijijini, kwahiyo soda za baridi zinanywewa vijijini. Ni maendeleo makubwa,” amebainisha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Mhe. Goodluck Mlinga, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga pesa nyingi kwa ajili ya kusambaza umeme katika Wilaya hiyo.
“Wilaya ya Liwale imepata zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini. Tulikuwa na vijiji 37 ambavyo havijapata umeme, Mhe. Rais ametoa pesa na leo hii Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini amefika Liwale kututhibitishia mpaka kufikia Desemba 30, vijiji vyote vitakuwa vinawaka umeme.”
Kiongozi wa Ujumbe huo, Meja Jenerali Kingu ametoa wito kwa wananchi wa Lindi na kote nchini ambako miradi ya umeme vijijini inatekelezwa, kutunza miundombinu ya umeme na kuachana na tabia ya kuichoma au kufanya uharibifu wa aina yoyote kwani inarudisha nyuma jitihada za Serikali za kuwapatia wananchi maendeleo.
“Katika kikao chetu na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Lindi, wamebainisha uharibifu wa miundombinu kuwa ni moja ya changamoto wanazokutana nazo. Nawasihi wananchi kuacha mara moja tabia hiyo kwani umeme ambao tunawapelekea ni kwa ajili ya manufaa yao wenyewe kiuchumi, kiusalama na kijamii,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mhandisi Olotu, Wakala wa Nishati Vijijini unatekeleza Miradi minne mkoani Lindi ambayo ni pamoja na REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotekelezwa katika vijiji vyote na Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B unaotekelezwa kwenye vitongoji.
Mingine ni mradi maalumu wa kupeleka umeme kwenye migodi midogo ya madini na maeneo ya kilimo pamoja na mradi maalumu kwa ajili ya vituo vya afya na pampu za maji.