Baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Mbao kijiji cha Ntungwa kata ya Mkomba Halmashauri ya wilaya Momba mkoani Songwe,wakichota maji katika moja ya vituo vinavyotoa huduma ya maji ya bomba vilivyojengwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) ambapo kwa mara ya kwanza tangu Uhuru mwaka 1961 wanancho wa kijiji hicho wamemepata mradi wa maji ya bomba.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Mbao katika kijiji cha Ntungwa wilaya ya Momba mkoani Songwe Christopher Simponda kulia,akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kitongoji hicho Peregia Aloyce,katikati anayeshuhudia ni kaimu meneja wa Ruwasa wilayani Momba Mhandisi Beatus Katabazi.
Tenki lenye uwezo wa kuchukua lita 100,000 za maji linalohudumia zaidi ya wakazi 1,100 wa kitongoji cha Mbao kijiji cha Ntungwa wilayani Momba lililojengwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa).
Na Muhidin Amri
Momba
ZAIDI ya wananchi I,100 wa kijiji cha Ntungwa kata ya Mkomba wilaya ya Momba mkoani Songwe,kwa mara ya kwanza wameanza kupata maji safi na salama baada ya serikali kutoa Sh.milion 210 kujenga mradi wa maji.
Wananchi wa kijiji hicho, wameishukuru serikali kuwezesha kupatikana kwa mradi wa maji ambayo hawajawahi kuyaona tangu kilipoanzishwa miaka ya 80 na kueleza kuwa huo ni ukombozi mkubwa katika maisha yao.
Benedict Marekani mwenye umri wa miaka 70 alisema,hawakuwahi kufikiria kwamba ipo siku watapata maji ya bomba,na kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa jitihada zake kwa kujenga na kukamilisha mradi huo.
Alisema,wakati wa masika hali ilikuwa mbaya kwani visima vyote vya asili na mito waliyoitegemea kupata maji ilijaa takataka na vinyesi vya wanyama,hali iliyosababisha baadhi ya watu kukaa muda mrefu bila kuoga na wengine kupatwa na maradhi ya tumbo.
Peragia Aloyce alisema,kabla ya kutekelezwa kwa mradi huo walikuwa wanaamka usiku wa manane na wakati mwingine hata kulala mtoni kusubiri maji,hali iliyochangia migogoro ya mara kwa mara kwenye ndoa zao.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Christopher Simponda alisema,changamoto ya huduma ya maji safi na salama ilisababisha hata kufungwa kwa shule ya msingi kutokana na wanafunzi kushindwa kupata baadhi ya huduma muhimu ikiwemo ya chakula na choo.
Ameipongeza serikali,na wataalam wa Ruwasa wakiongozwa na kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Momba Beatus Katabazi, kwa kazi nzuri ya kutekeleza mradi huo uliomaliza kabisa adha ya huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji chake.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Momba mkoani Songwe Beatus Katabazi alisema,awali wananchi wa eneo hilo walikuwa na adha kubwa ya huduma ya maji safi na salama licha ya kuwa miongoni mwa maeneo yenye shughuli nyingi za kibinadamu.
Alisema,kutokana na adha hiyo serikali iliamua kutenga Sh.milioni 276 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo,hata hivyo kutokana na kutekelezwa na mafundi wa ndani fedha zilizotumika ni Sh.milioni 210, hivyo kuokoa Sh.milioni 66 ambazo zilielekezwa kwenye maeneo mengine yenye changamoto ya maji.
Alisema,mradi huo una uwezo wa kuhudumia wananchi wa kijiji hicho hata kwa miaka ishirini ijayo kwa sababu maji yaliyopo ni mengi ikilinganisha na idadi ya watu waliopo.
Katabazi alitaja kazi zilizotekelezwa katika mradi huo, ni ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 100,000 na mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 2.5 na kujenga vituo 5 vya kuchotea maji.
Aidha alisema,tangu mradi ulipoanza kutoa huduma zaidi ya watu 10 wameshaunganishiwa huduma ya maji majumbani na hivyo kupunguza adha ya kukaa kwa muda mrefu kwenye vituo vya kuchotea maji.
Katabazi alieleza kuwa,kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wametenga Sh.milioni 200 kwa ajili ya kununua mabomba madogo na mita(dira) kwa ajili ya wateja wa majumbani ili kuwapunguzia wananchi gharama ya kuingiza maji kwenye nyumba zao.
Katika hatua nyingine Katabazi alieleza kuwa, kabla ya mwezi Disemba mwaka huu Ruwasa itaanza kugawa mabomba kwenye maeneo yenye miradi ili kuwasaidia wananchi waweze kuungnishiwa huduma ya maji safi na salama kwenye nyumba zao.