Afisa utumishi wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)mkoa wa Songwe Bahati Nyamadyaki kushoto,akimtua ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Maheche wilaya ya Ileje mkoani humo Sara Mayola,baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji safi na salama wa Ntembo -Msia uliotekelezwa na Ruwasa kwa gharama ya Sh.milioni 455.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ntembo wilaya ya Ileje mkoani Songwe, wakimsikiliza afisa utumishi wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)mkoa wa Songwe Bahati Nyamadyaki kulia, baada ya kutembelea mradi wa maji wa Ntembo-Msia unaokwenda kuwanufaisha zaidi ya wakazi 13,326 wa kata ya Ntembo na Msia.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Iyuli wilaya ya Ileje mkoani Mbeya Alen Mahuli katikati akiwaelekeza baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo namna ya matumizi ya maji ya bomba baada ya kufikisha huduma ya maji safi na salama ambayo yamewezesha wanafunzi kupata muda mwingi wa masomo.
Na Muhidin Amri,
Ileje
WITO umetolewa kwa wakazi wa kijiji cha Mshinji kata ya Mbebe wilaya ya Ileje mkoani Songwe,kuwa na tabia ya kulipia gharama za maji ili fedha zinazokusanywa zitumike katika kuimarisha na kuboresha huduma ya maji katika maeneo yao.
Hayo yamesemwa jana na afisa utumishi wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)mkoa wa Songwe Bahati Nyamadyaki,wakati akizungumza na wananchi wa kijiji hicho baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji.
Alisema,ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha analipia gharama za maji anayotumia kwani miradi hiyo inahitaji kujiendesha kupitia vyombo vya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO)ili iweze kutatua changamoto ya maji na kudumu kwa muda mrefu.
Alisema,suala la kulipa ankara za maji, ulinzi wa miundombinu na vyanzo vya maji likiachwa kufanywa na serikali peke yake ni kutengeneza jamii isiyowajibika,kwa hiyo kila mmoja anapaswa kuwajibika katika ulinzi wa vyanzo na kutoa taarifa pale miundombinu ya maji inapoharibika.
Mwakilishi wa Ruwasa wilaya ya Ileje Sifa Edom alisema,mradi wa maji Shinji umegharimu zaidi ya Sh.milioni 496 ambazo zimetumika kujenga chanzo cha maji,kujenga tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000 ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 6 kuchimba mtaro na kulaza bomba.
Alisema,mradi huo una uwezo wa kuhudumia takribani watu 10,000 lakini kwa sasa umeanza kuhudumia watu 2,594 wa kijiji cha Mshinji,hivyo kijiji hicho kuwa na akiba ya maji yanayoweza kutumika kwa muda wa miaka 10 ijayo.
Ameishukuru serikali kutoa fedha zilizowezesha kutekeleza mradi huo uliowasaidia wananchi wa kijiji cha Mshinji kuondokana na adha ya kutumia maji ya visima pamoja na wanyama wa kufugwa kama ng’ombe na wanyama wa porini wakiwemo nguruwe.
Aidha Edom alisema,serikali imetoa Sh.milioni 455,715,106.47 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji wa Mtembo-Msia utakaohudumia zaidi ya watu 15,000 wa vijiji 7 katika kata ya Chitete na Mlale.
Alisema,katika mradi huo wamejenga vituo 6 vya kuchotea maji,matenki mawili madogo kwa ajili ya kupunguza kasi ya maji na kuuongezea nguvu mradi wa zamani ambao kwa sasa uwezo wake wa kutoa huduma ya maji imepungua.
Alisema,vijiji viwili ni vya kata ya Mlale na vijiji vitano kata ya Chitete ambapo mradi unaendelea kutekelezwa na tayari watu 4,870 wameanza kunufaika na unaotarajia kukamilika mwezi Disemba mwaka huu.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mbebe John Mtafya,ameishukuru serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kupeleka huduma ya maji ya bomba katika vijiji vyote vinne vya kata hiyo.
Alisema,hiyo ni hatua kubwa kwa serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwani imewasaidia wananchi wa kata ya Mbebe kutumia maji hayo katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mkazi wa kijiji cha Mtembo Lucia Mwampasa alisema,kwa muda mrefu kijiji hicho hakikuwa na mradi wa maji ya bomba badala yake walilazimika kutumia maji ya visima na hivyo kusababisha kero kubwa hasa kutokana na kutumia muda mrefu wanapokwenda kuchota maji.
“mradi huu umetusaidia sana kupata nafasi ya kufanya shughuli nyingine za kiuchumi,kwani hapo awali tulitumia kati ya masaa 2 na matatu kwa ajili ya kwenda kutafuta maji kwa matumizi ya familia zetu”alisema.
Amini Mkimbira alisema,kabla ya mradi huo ndoa zao zilikuwa mashakani hasa kwa wanawake wanapochelewa kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji,lakini sasa wanafuraha kupata mradi wa maji ya bomba uliowezesha kuimarika kwa ndoa na uchumi wa familia.