*******************************
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Hatimaye Bibi Somoye Dadi Dabali aliyekuwa akidai shamba lake kwa muda imeamuliwa leo arejeshewe shamba lake alilochukuliwa na Mjukuu wake Sofina Salum Said Liuma.
Maamuzi hayo yamefanywa na Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu mara baada ya kuzikutanisha pande zote za mshtaki, mshatakiwa na mashahidi wao na kuridhishwa Bibi Somoye apewe ardhi hiyo ambayo alimpa Mjukuu wake huyo alime Mihogo kwa muda naye Mjukuu Sofina akaamua kupanda Mikorosho ambayo ina mwaka mmoja sasa wakati ambao Bibi Somoye alikuwa anaumwa.
Baadae Mjukuu Sofina alitaka kumlipa Tsh. Laki sita Bibi yake huyo Somoye ili amwachie shamba naye Bibi akakataa na kusema Sofina arudishe shamba lake na hahitaji hela yake kwani ameonyesha utovu wa nidhamu wa kutaka kumdhulumu shamba.
*”Nimesikiliza pande zote vizuri na leo ninaamuru Sofina kurejesha ardhi ya Bibi Somoye na isitokee Bibi huyo kusumbuliwa kwa namna yeyote ile. Kuanzia sasa Shamba liwe mikononi mwa Bibi Somoye”* Alisisitiza Gavana Shilatu.
Katika hatua za kusikiliza kesi hiyo Gavana Shilatu aliambatana na Mtendaji Kata Miuta, Mtendaji Kijiji cha Ng’ongolo lililo shamba hilo, Mashahidi pamoja na Wajumbe wa Baraza la ardhi la Kata.