Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Resani Mnata (kushoto) akipokea tuzo ya heshima ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoka kwa Mratibu wa Tamasha la Yamnyausi Organization for Arts and Sports (YOAS) Bw. Stewart Mwaluko (kulia) wakati wa hafla ya kufunga tamasha la Utamaduni la Asili Yetu la Mkoa wa Dodoma Novemba 8, 2023 jijini Dodoma. Katikati ni Mgeni Rasmi wa hafla hiyo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Dkt. Noelia Muyonga.
Na Eleuteri Mangi, WUSM
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Dkt. Noelia Muyonga amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwalea watoto na vijana kujifunza mila na desturi zilizo njema ili kuendeleza utamaduni wa mtanzania.
Dkt. Noelia ametoa kauli hiyo Novemba 8, 2023 jijini Dodoma wakati akifunga tamasha la Utamaduni la Asili Yetu la Mkoa wa Dodoma ambalo limejumuisha vikundi 27 vya ngoma za asili kutoka wilaya zote za mkuoa huo.
“Nimefurahishwa sana nilipoona vikundi vilivyo ‘perform’ leo, mmefanya vizuri sana kuwaleta watoto, watoto walikuwa wanapiga ngoma kwa ufasaha kabisa na kufurahia. Kwa hiyo tuwatie moyo tunapohamasisha watoto kupenda ngoma za asili na maadili yanaendanda na mila na desturi zilizo njema, hatuwezi kutenganisha Utamaduni, Sanaa na Utalii” amesema Dkt. Noelia.
Dkt. Noelia amesisitiza kuwa utamaduni ni zao la utalii ambalo watalii wengi wanavutiwa nalo ikizingatiwa kuwa wanajua Tanzania kuna Wanyama, fukwe pamoja na mapori vitu ambavyo vimezoeleka vinapatikana hapa nchini.
Ameongeza kuwa “Tuendelee kuhamisha kwa bidi zetu zote utalii huu uhamie kwenye utalii wa kiutamaduni, maana tuna utajiri mkubwa kwenye mikoa yote maana kuna makabila zaidi ya 120 hapa nchini, tukisimama kwa pamoja tukatangaza kila mahali mil ana utamaduni wetu, tutaongeza thamani ya Utalii hapa kwetu Tanzania.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi kwenye tamasha hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni Dkt. Resani Mnata amesema mchanganyiko wa washiriki wa tamasha hilo ambao unajumuisha Watoto, wanafuinzi wa shule za msingi na sekondari pamoja na wageni wengine umepangwa hivyo kwa lengo la tamasha hilo ni kuiwarithisha Watoto, vijana watu wengine kuujua na kuendeleza urithi wa utamaduni kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Mratibu wa Tamasha la Yamnyausi Organization for Arts and Sports (YOAS) Bw. Stewart Mwaluko tamasha hilo linahusisha ngoma za asili kutoka katika Wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma na kupata vikundi vitatu ambavyo ndivyo vilishinda katika Wilaya zao ikiwa ni hatua ya kutangaza vivutio vilivyopo mkoa wa Dodoma.