Mwenyekiti wa kijiji cha Mwakizega Jafery Abdala kulia,akimsikiliza Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma Sudi Dibwine katikati, kuhusiana na kusuasua kwa ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji hicho unaotekelezwa kwa fedha za mfuko wa Taifa wa maji,kushoto mhandisi wa Ruwasa kutoka ofisi ya meneja wa Ruwasa wilaya ya Kigoma Aron Kaje.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma Mhandisi Sudi Dibwine aliyenyoosha mkono,akiwaonyesha baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji cha Mwakizega kata ya Mwakizega wilayani humo mabomba yatakayotumika kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji hicho.
Na Muhidin Amri-Uvinza
BAADHI ya wanawake wa kijiji cha Mwakizega wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma,wameiomba serikali kukamilisha haraka ujenzi wa mradi wa maji unaotekelezwa katika kijiji hicho ili kuwapunguzia adha kwa kutembea umbali mrefu na kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji huku wakiwaacha waume zao kitandani.
Walisema,wanalazimika kuamka usiku na kutembea zaidi ya kilomita 2.5 kwenda Ziwa Tanganyika kufuata maji,hivyo kuziweka ndoa zao na uhai wao mashakani kwa kuwa wanapita kwenye maeneo yenye wanyama wakali wakiwemo mambo na viboko.
Jenisia Amlani alisema,kero inakuwa kubwa zaidi hasa kwa mama wajawazito wanapokwenda Hospitali kujifungua, kwani yanahitaji maji ya mengi kwa ajili ya masuala ya usafi wa mwili na nguo.
“natoka nyumbani saa sita usiku kwenda kuchota maji ziwa Tanganyika na kurudi saa 10,mwanaume gani anaweza kuvumilia hali hiyo,tunaiomba serikali inayoongozwa na mwanamke mwenzetu mama Samia iharakishe ujenzi wa mradi wetu wa maji ili tuweze kuondokana na kero hii”alisema.
Neema Joshua alisema,wanatumia muda mwingi kufika ziwa Tanganyika kufuata maji, muda ambao wangeweza kutumia kufanya kazi nyingine za maendeleo badala ya kupoteza kwa kwenda kutafuata maji.
“mradi huu ulioanza kutekelezwa miaka mitatu iliyopita lakini hadi sasa haujakamilika,sisi wananchi tunashida kubwa ya maji hali inayosababisha tukose muda wa kufanya shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo”alisema Joshua.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mwakizega Jafery Abdala alisema,kijiji hicho chenye wakazi 16,822 tangu kilipoanzishwa mwaka 1974 hakijawahi kupata maji ya bomba,badala yake wananchi wanatumia maji ya ziwa Tanganyika na maji kutoka kwenye vyanzo vya asili ambayo sio safi na salama.
Alisema,wanaendelea kuteseka kwa kukosa huduma ya maji safi na salama huku baadhi yao wanapata maji kwenye nyumba za ibada(msikitini na kanisani) ambako viongozi wa taasisi hizo wameruhusu wananchi kuchota maji kwa kulipia fedha.
Alisema kutokana na kusua sua kwa ujenzi wa mradi huo,wananchi wameanza kukata tamaa ya kupata mradi wa maji ya bomba licha ya serikali kupitia Waziri Mkuu kuhaidi kijiji hicho kitapata mradi wa maji ya uhakika.
Ameiomba serikali,kuhakikisha inatoa fedha zote zilizopangwa kukamilisha mradi huo ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2020 ili kuwanusuru wananchi na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama kwenye makazi yao.
Kwa upande wake kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Uvinza Sudi Dibwine alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi Februari mwaka 2020 kufuatia agizo la Waziri mkuu Kassim Majaliwa wakati wa ziara yake wilaya humo.
Alisema,changamoto katika utekelezaji wa mradi ni fedha zake kuletwa kwa awamu kutoka mfuko wa Taifa wa maji,hivyo inakuwa vigumu kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa.
Alisema,makadirio ya fedha za ujenzi wa mradi huo ni Sh.bilioni 1.2 lakini wamepokea Sh.milioni 725 zilizotumika kuchimba kisima chenye urefu wa mita 80,kujenga tenki,kuchimba mitaro na kulaza mabomba umbali wa kilomita 23 kati ya kilomita 24.
Alitaja kazi zilizobaki ni kulaza bomba kuu kutoka Ziwa Tanganyika hadi kwenye tenki,kulaza bomba kutoka kwenye tenki hadi kwenye makazi ya wananchi umbali wa kilomita 1.4 na tayari bomba kwa ajili ya kusambaza maji kwenda kijijini zimefika na kazi itaendelea ili kukamilisha ujenzi huo.
Alisema,ni matarajio ya Ruwasa kwamba ifikapo mwezi Januari mwaka 2024 mradi huo utaanza kutoa huduma na kumaliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wa kijiji hicho kukosa huduma ya maji safi na salama kwenye makazi yao.