Serikali Tarafa ya Mihambwe mkoani Mtwara imekitaka Chama cha msingi cha ushirika cha Chifike Amcos kulipa zaidi ya Tsh. milioni tano wanazodaiwa na Vijiji.
Hayo yamejitokeza kwenye mkutano wa Kijiji cha Chikongo baada ya kubainikia chama hicho hakijapeleka fedha katika Vijiji vya Misufini na Chikongo kutokana na makato ya ushuru wa korosho mwaka 2017/2018
Hilo limebainika baada ya taarifa ya mapato na matumizi kusomwa kwenye mkutano mkuu wa hadhara wa kijiji hicho.
Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu aliyehudhuria mkutano huo aliupa siku tatu uongozi wa Amcos kuitisha kikao cha bodi kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa.
Shilatu ameitaka Bodi ya Amcos kuitisha kikao, kujadili hatimaye kulipa fedha hizo za ushuru kwa Vijiji vya Misufini na Chikongo.
*”Itisheni kikao cha Bodi haraka. Jadilini jinsi mtakavyovilipa makato ya mauzo ya korosho, Fedha hizo si zenu ni za vijiji. Viongozi heshimuni taratibu za kisheria acheni ubabe na ulaghai.”* Alisema Gavana Shilatu
Alisema vyama vya ushirika visiwe ni vichaka vya kuficha wahalifu na wahujumu uchumi bali visaidie kusukuma mbele maaendeleo ya kilimo na kulinda maslahi ya wakulima.
Wakati huo huo Gavana Shilatu aliwataka Wanakijiji kuendelea kusalimisha mifuko ya plastiki kwenye ofisi ya Kijiji au ya kata.
Pia aliwakumbusha wajasirimali wadogo wasio na vitambulisho kuhakikisha wanavilipia ili kuwa navyo kwenye shughuli zao za kila siku kama agizo la serikali lilivyoelekeza.
Katika mkutano huo wa Kijiji ulihudhuliwa na Diwani kata ya Mkoreha, Mtendaji kata ya Mkoreha pamoja na Afisa wa Tarafa Mihambwe