Tenki jipya kulia lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 za maji lililojengwa katika mradi wa maji Usunga wilaya ya Sikonge mkoani Tabora,kushoto ni tenki la zamani lililokuwa linahudumia wakazi wa kijiji hicho.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Usunga wilayani Sikonge wakichota maji katika moja ya vituo vilivyojengwa katika mradi huo.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Sikonge mkoani Tabora Mhandisi Fikiri Samadi,akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Usunga wilayani humo Nelia Andrew.
Na Muhidin Amri
Sikonge
WIZARA ya maji kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilayani Sikonge,imetumia zaidi ya Sh.milioni 260 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji cha Usunga na Urafiki kata ya Usunga wilayani humo.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Sikonge Fikiri Samadi alisema,mradi wa maji Usunga ulisanifiwa ili kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho ambao kwa muda mrefu hawakuwa na maji ya uhakika.
Alisema,chanzo cha mradi huo ni kisima kirefu kilichochimbwa na Shirika la msaada la Japani(JAICA)tangu miaka ya themanini chenye uwezo wa kuzalisha lita za maji 4,200 kwa saa moja.
Samadi alitaja kazi zilizofanyika katika utekelezaji wa mradi huo ni kuboresha kisima,kujenga mtandao wa maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye tenki,kujenga tenki la lita 50,000 na kujenga vituo 9 vya kuchotea maji katika maeneo mbalimbali.
Alisema baada ya mradi kuanza kutoa huduma,wananchi wengi wamehamasika na kuvuta maji majumbani na hivyo kupunguza msongamano kwenye vituo na kuunga mkono kauli mbiu ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua ndoo mama kichwani.
Aidha alisema,Ruwasa imetumia Sh.milioni 40 kufikikisha mtandao wa maji safi na salama kijiji cha Urafiki ambacho wananchi wake walitembea umbali wa kilomita 4 kwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili.
Akizungumzia upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya ya Sikonge Samadi alisema,kabla ya kuanzishwa kwa Ruwasa huduma ya maji ilikuwa asilimia 47,lakini kutokana na jitihada za serikali kupitia Ruwasa imefanikiwa kutekeleza jumla ya miradi 7 na kati ya hiyo miradi 5 imekamilika na inatoa huduma ya maji.
Alisema,miradi hiyo imewezesha kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 47 hadi kufikia asilimia 53.4 na wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia vyanzo ikiwemo visima virefu,mabwawa na chemchem.
Alitaja baadhi ya miradi hiyo ni mradi wa Mwamayunga, ambao maji yake yanatoka bwawa maarufu la Utyatya unaokwenda kunufaisha vijiji vinne vya Mwamayunga kata ya Kibanga,Urafiki,Isanyandugu na Usunga.
Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Hamis Kimwaga alisema,kabla ya mradi huo kwa siku ofisi yake ilikuwa inapokea kesi kati ya 7 hadi 10 kutoka kwa wanawake hasa walioko kwenye ndoa wakilalamika kupigwa na waume zao kwa sababu ya kuchelewa kurundi nyumbani wanapokwenda kutafuta maji.
Mkazi wa kijiji hicho Nelia Andrew,ameishukuru serikali kuwajengea mradi huo ambao ni msaada mkubwa na chachu ya mafanikio katika maisha yao.
Alisema,sasa wanapata muda mwingi wa kushiriki kikamilifu katika kazi za maendeleo tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wanatumia muda wa masaa 2 kwenda kutafuta maji .