Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu,akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 3,2023 jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa kamati huru kuhusu ufaulu wa mitihani ya watarajali inayoendeshwa na Baraza la Madaktari Tanganyika.
Na WAF – DODOMA
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameliagiza Baraza la Madaktari Tanganyika kuendelea kuendesha mitihani miwili ya kabla na baada ya Utarajali kwa Madaktari wote nchini wanaomaliza vyuo na kuuanza mafunzo kwa vitendo.
Waziri Ummy amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa kamati huru kuhusu ufaulu wa mitihani ya watarajali inayoendeshwa na Baraza la Madaktari Tanganyika kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati Prof. Mohammed Kambi.
Waziri Ummy amesema Daktari yeyote aliyemaliza masomo yake katika vyuo vya udaktari ndani na nje ya nchi ili apate leseni ya Udaktari ni lazima afanye mtihani wa kabla ya utarajali na baada ya kukamilisha kipindi cha utarajali.
Aidha, Waziri Ummy amelitaka Baraza la Madaktari Tanganyika kuzingatia miongozo ya alama za ufaulu kama ilivyoelekezwa ili kusimamia taaluma ya Udaktari na endapo Daktari atashindwa kufikia alama zilizopendekezwa kwenye muongozo itabidi arudie mitihani.
Waziri Ummy ameliagiza Baraza la Madaktari Tanganyika kutoruhusu daktari aliyefeli Mtihani wa utarajali kuendelea na mafunzo kwa vitendo badala yake itamlazimu arudie mtihani huo mpaka afaulu ndipo aendelee na mafunzo kwa vitendo (Internship).
Kwa upande mwingine Waziri Ummy amesema Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu pamoja na na vyuo na taasisi za Ithibati ili kuboresha mafunzo kwa upande wa Madaktari wakiwa vyuoni.
Waziri amesema Wizara ya Afya itaendelea kutimiza jukumu la kumlinda Mwananchi kwa kuhakikisha anapata huduma bora kutoka kwa wanataaluma wa Afya waliothibitishwa na Mabaraza ya kitaaluma kuwa ulinganifu na ubora unaotakiwa utakaowezesha kutoa huduma za afya bora kwa wananchi.
Akiwasilisha mapendekezo ya Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo prof. Mohammed Kambi amesema Kamati imependekeza mitihani ya utarajali kuendelea kufanyika licha ya madaktari kulalamikia ufaulu mdogo huku akilitaka Baraza la Madaktari Tanganyika kutoa alama za ufaulu kwa madaktari waliofanya mitihani hiyo.