Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mlele mkoani Katavi Mhandisi Madaha Majagi,akionyesha sehemu ya bwala Nsekwa litakalotumika kuzalisha maji kwa wakazi wa vijiji 16 vya wilaya hiyo.
Baadhi ya akina mama wa kijiji cha Nsekwa wilayani Mlele wakiwa na ndoo wakienda kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili kwa ajili ya matumizi ya familia zao.
Na Muhidin Amri,
Mlele
ZAIDI ya wakazi 65,000 wa kata tano wilaya ya Mlele mkoani Katavi, wanatarajia kunufaika na mradi wa Bwala la kuvuna maji ya mvua la Nsekwa,unaotekelezwa na serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa).
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mlele Madaha Majagi alitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni Inyonga,Kalovya,Kamalampaka Utende,Mgombe,Kanoge na Wachawaseme,Mtakuja,Nsekwa, Kaulolo,Ipwaga,Mapili,Masigo,Kamsisi,Imalaunduki na Songambele.
Majagi alisema, kwa sasa wakazi wa vijiji hivyo wanategemea kupata huduma ya maji kupitia visima virefu(bore holes)ambavyo havitoshelezi mahitaji,hivyo mradi huo utamaliza kero ya maji safi na salama katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Majagi,mahitaji ya maji katika vijiji hivyo ni lita za ujazo milioni 449.5 kwa mwaka,lakini bwawa hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhifadhi takribani lita bilioni 2.8 za maji,hivyo kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 83.9 hadi kufikia asilimia 95.
Alisema,bwawa hilo ni chanzo muhimu cha maji kwani linakwenda kumaliza kabisa adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji hivyo ambao wanatembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.
Aidha alisema,mradi huo ni mkombozi kwa wakazi wa wilaya ya Mlele kwani utahudumia eneo kubwa na utakuwa sehemu maalum ya kunywea mifugo ili kuepusha uwezekano wa uharibifu wa vyanzo vya maji vilivyopo.
Aliongeza kuwa,awali bwawa hilo lenye ukubwa wa ekari 47 lilitengwa kwa ajili ya hifadhi ya chanzo cha maji,lakini kutokana na umuhimu wake Serikali imeamua lijengwe na kuboreshwa zaidi ili kuwa chanzo kikubwa cha maji.
Alitaja kazi zilizofanyika kwenye utekelezaji wa mradi ni ujenzi wa tuta lenye urefu wa mita 650,utoro wa maji,vituo vya kuchotea maji,ulazaji na ufukiaji wa bomba na kujenga nyumba ya msimamizi wa mitambo ya kusukuma maji.
Alisema, kwa sasa kazi zilizobaki kabla ya kuanza matumizi ya bwawa hilo ni ujenzi wa chujio ambao haujaanza lakini upo hatua ya manunuzi.
Mkazi wa kijiji cha Nsekwa Neema Anton alisema,ujio wa mradi huo ni jambo la faraja kubwa, kwani utamaliza changamoto ya huduma ya maji safi na salama iliyokuwepo kwa muda mrefu.
Josephine Christopher alisema,katika kijiji hicho kuna mradi wa maji uliojengwa miaka ya themanini,hata hivyo miundombinu yake imechakaa na kuanza kuharibika,kwa hiyo mradi wa maji ya bwawa utasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji na kumaliza kero ya huduma hiyo.