Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe.Angellah Kairuki akizungumza katika mkutano huo mkoani Arusha.
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha. Zaidi ya Wataalamu wa sekta ya misitu na wanyamapori wapatao 300 kutoka nchi 53 Afrika wamekutana mkoani Arusha kwa lengo la kujadili maswala ya mabadiliko ya tabia ya nchi iliyokumba dunia na kutafuta muafaka namna ya kukabiliana nayo.
Majadiliano hayo yanafanyika kwa siku tano mfululizo katika mkutano wa 24 wa Kamisheni ya Afrika inayosimamia misitu na wanyama pori (AFWC24) ulioandaliwa na shirika la kilimo na chakula duniani(FAO) na Serikali ya Tanzania ikiwahusisha wakurugenzi, mawaziri na watafiti kutoka nchi hizo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo Prof.Dos Santos Silayo amesema kuwa,majadiliano haya yanalenga kubadilishana uzoefu juu ya mabadiliko ya tabia ya nchi lakini pia kuweka sera na mkakati wa pamoja wa kukabiliana nayo hasa katika sekta za misitu na wanyama pori ili kunusuru rasilimali hizo lakini pia nchi inufaike nayo.
“Mkakati huo tutakaojiwekea unalenga pia na kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi, Maswala ya ujangili, Uvunaji wa misitu usiozingatia taratibu pia Changamoto za moto katika maeneo ya hifadhi lakini pia Kuangalia fursa za kibiashara ambazo rasilimali hizi zinaleta ili zichangie kwenye maendeleo ya nchi ambazo zipo” amesema.
Naye Waziri wa maliasili na utalii, Angellah Kairuki amesema kuwa wana matumaini makubwa Tanzania kunufaika na mkutano huo katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabia ya nchi hasa katika kupata uzoefu wa nchi zingine nini wanafanya kunufaika kwa rasilimali walizonazo ili Tanzania nayo iweze kuchukua hatua.
“Kwa sasa dunia inaegemea kuokoa anga dhidi ya hewa chafu ya cabon hivyo kama Tanzania tuna mikakati kabambe ya kuhakikisha hatupitwi na fursa hii hivyo tumeleta wataalamu wengi katika mkutano huu wajifunze biashara hii ya hewa ya ukaa na kuleta mapendekezo”amesema .
Amesema wa sasa serikali imeweka mikakati ya kujumuisha hifadhi za Taifa na mamlaka za hifadhi ikiwemo Tanapa, Ngorongoro, TAWA, TFS na zingine kuangalia namna ya kupanda miti mingi itakayoongeza kiwango cha unyonyaji wa hewa hii angani ili nchi iweze kujipatia kipato kikubwa kupitia biashara hii”
Alisema kuwa kupitia mpango huo, Tanzania itaweza kukabiliana na mabadiliko ya Tabia ya nchi, lakini pia kuongeza Pato la Taifa na zaidi kuondoa hewa na cabon hadi kiwango sifuri ifikapo mwaka 2050 .
Awali, Afisa misitu na wanyama pori kutoka shirika la kilimo na chakula duniani (FAO) Afrika, Edward Kilawe alisema kuwa lengo la kuandaa mkutano huo ni kusaidia nchi zote za Afrika kamisheni ya misitu na wanyama pori kujadili namna ya Kunyayua sekta hizo na Kuangalia changamoto mbali mbali zinazoikabili na kupanga namna ya kutatua.
“Mbali na hilo tunataka kujua changamoto za pamoja wanazokumbana nazo katika kukabiliana na uokoaji wa misitu na hifadhi za wanyama pori ili tuweze kuungana na mashirika mengine kuwasaidia ili kufanya Afrika kuwa na uhakika wa chakula”