Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye Mkutano wa Kimataifa wa 23 wa Baraza la Utalii Duniani (WTTC) unaofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kigali (Kigali Convention Centre) nchini Rwanda.
…………….
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezisihi nchi za Afrika kuandika upya kuhusu bara la Afrika kwa kuelezea simulizi zao wenyewe.
Ameyasema hayo katika Mkutano wa Kimataifa wa 23 wa Baraza la Utalii Duniani (WTTC) uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano nchini Rwanda.
Rais Samia amesema serikali za Afrika lazima zijitafakari upya ili utalii uweze kushamiri ikiwemo kujitangaza kimkakati, kufanya utafiti na uhifadhi.
Akisisitiza hilo, Rais Samia amesema katika zama hizi za taarifa potofu, Afrika haitakiwi kukaa kimya na badala yake ieleze ukweli wa bara hilo kwani muda ni sasa.
Aidha Rais Samia amesema iwapo kweli Afrika ikitaka kuendelea kuwa na vivutio vya asili ni lazima itoe kipaumbele kwenye uhifadhi na kuunga mkono jitihada za kutunza maeneo ya kiutamaduni, kazi za sanaa hususan za kihistoria na mila kwa vizazi vijavyo.
Utafiti, vivutio kwenye masuala ya utalii na athari za mazingira ni muhimu kwenye sekta hiyo ili umuhimu wake ubaki barani Afrika.
Wakati huo huo, Rais Samia amesisitiza wajibu wa sekta binafsi kwenye mfumo mzima wa utalii akihimiza umuhimu wa kuwepo ushirikiano baina ya serikali, sekta binafsi pamoja na asasi zisizo za serikali.
Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu