Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema limeanza oparesheni maalum ya kuwasaka wanafunzi wa vyuo vikuu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kama vile wizi na vile ambavyo ni kinyume na muenendo mwema wa maadili ya kitanzania.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga amesema hayo Alhamisi Novemba 2, 2023 wakati akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Mbeya .
“Mkoa wa Mbeya kuna tatizo la wanafunzi wa vyuo vikuu kujihusisha na vitendo vya uhalifu hususani wanafunzi wa mwaka wa kwanza na kusababisha kupoteza mwelekeo ”, alisema.
Aidha, Kamanda Kuzaga amekemea wanaume kuacha tabia ya mapenzi ya jinsi moja na kuwataka kuzingatia elimu iliyofanya wawepo Mbeya.
Pia amewataka wanawake kuacha tabia ya kujiuza kwani ni kinyume cha sheria na na kusema “mnapokula chipsi mayai za watu mnatarajia nini kinafuata ndio hayo ya kufanyiwa vitendo vya uzalilishaji na kinyume cha maadili” alisema.
Kwa Upande wake mlezi wa Wanafunzi Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Mbeya, Florence Kalimbikulu amemshukuru Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya kwa ujio wake ambapo aliweza kueleza baadhi ya changamoto ikiwepo ya “double parking” eneo la barabara ya Mzumbe kuelekea Mahakama kuu.
Naye, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Jamii na kaimu Mkuu wa Chuo, John Jorojick ameonya wanafunzi waliopata fursa ya masomo kwa mwaka wa kwanza kuepuka vitendo viovu ikiwepo ushoga, kujiuza miili na uhalifu.
“Kuna wanafunzi 1,500 wa mwaka wa kwanza katika fani mbalimbali pia tuombe hali ya usalama kuimarishwa katika eneo la chuo kwani kipindi cha likizo kuna kuwa hakuna matukio ya uhalifu lakini tukifungua uhalifu unakuwa mkubwa ambao baadhi ya wanafunzi kuhusishwa” alisema.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Jeshi la Polisi, Mkaguzi wa Polisi Loveness Mtemi amesema kwenye taasisi za elimu ya juu kuna changamoto lukuki za ukatili wa kijinsia na kuwataka wanafunzi wa mwaka wa kwanza kutoa taarifa pindi waonapo viashiri vya uhalifu au pindi yanapojitokeza matukio ya uhalifu na kuathiri masomo yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia yupo katika ziara ya kutembelea na kutoa elimu ya usalama kwa wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na vyuo kwa lengo la kuzuia uhalifu hasa unaojitokeza maeneo ya masomoni.