Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (katikati) akionesha magunia ya mkaa yaliyokamatwa baada ya kukiuka sheria ya misitu na nyuki katika msitu wa Sambalu mkoani Singida wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) eneo la tukio juzi. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ikungi (OCD), Fortunatus Biyacca na kulia ni Mshauri wa Jeshi la Akiba la wilaya hiyo, Kapteni Chabimia na kushoto ni Afisa wa Wakala wa Huduma ya Misitu (TFS)
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akiwa aamini anachokiona kufuatia uharibifu mkubwa wa mazingira wa ukataji wa miti na kuchoma mkaa. Kushoto huyo mama ni Mfanyabiashara wa mkaa Rose Nari, kutoka mkoani Arusha ambaye amekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Shehena ya magunia ya mkaa yaliyo kamatwa.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akisisitiza jambo eneo la tukio.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akiwaongoza wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya kukagua maeneo yaliyo haribiwa kwa kukatwa miti.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akisalimiana na mwananchi Baraka Musa ambaye anafanyashughuli za kilimo na ufugaji katika hifadhi hiyo ya Taifa ya Sambalu.
Hivi ndivyo hali ilivyo baada ya kukatwa miti katika hifadhi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akizungumza na moja ya familia inayoishi ndani ya familia hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akizungumza na na Balozi wa Mtaa wa Makulunde, Hamis Juma kuhusu uharibifu huo wa mazingira ambaye alisema wanakata miti hiyo na kuchoma mkaa ambao wanauza gunia sh.5000 kwa ajili ya kupata fedha za kununulia mahitaji yao mengine ya kila siku.
Miti ikiwa imekatwa.
Maofisa wa TFS wanaohusishwa na tukio hilo wakiwa eneo la tukio. Kutoka kushoto ni Selemani Elifuraha na Isack Maluma aliyekutwa akimkabidhi stakabadhi ya malipo mfanyabiashara huyo.
Mfanyabiashara wa mkaa, Rose Nari, akizungumza na waandishi wa habari alisema wakati katazo hilo lilipokuwa linatoka mkaa huo ulikuwa umechomwa tayari.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imetaifisha magunia ya mkaa 121 yaliyokamatwa wakati yakitaka kusafirishwa kwa njia za ujanja baada ya kukiuka taratibu za sheria ya misitu na nyuki.
Na katika hatua nyingine serikali wilayani hapa imeomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kulichunguza tukio hilo ilikuweje vitolewe vibali vya kusafirisha mkaa huo wakati kulikuwepo na katazo na wamevitaka vyombo vya dola kumchukulia sheria mfanyabiashara aliyekamatwa na mkaa huo pamoja na maofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wilayani hapo waliohusika kutoa vibali hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi mbele ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo eneo la tukio katika Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Sambalu uliopo Kata ya Mang’onyi ambapo magunia hayo ya mkaa yalikamatwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo alisema kitendo hicho ni kibaya sana na kimekiuka sheria ya misitu namba 14 na namba 15 ya nyuki ni kitendo ambacho kinaathiri mazingira.
Alisema kwa mujibu wa sheria za misitu na uanzishwaji wa TFS ya mwaka 2010 kitendo walichokifanya hao maofisa wa TFS ni kinyume na taratibu kwani wao wametoa vibali vya kusafirisha mkaa huo wakidai ni kwa ruhusa yangu wakati sio kweli.
“TFS walikwenda polisi kuomba kibali cha kutaka wapewe askari kwa ajili ya kusindikiza mkaa huo kwenda mjini Singida kwa mauzo wakidai nimetoa kibali hicho wakati sio kweli nimempongeza mkuu wa polisi wa wilaya kwa kunishirikisha kwa kuniuliza” alisema Mpogolo.
Alisema baada ya kufika kituoni hapo aliwakuta maofisa hao wa TFS wakiwa tayari wamemuandikia risti mfanyabiashara huyo na ndipo walipowakamata na siku iliyofuata kamati nzima ya ulinzi na usalama wilayani hapo ilikwenda katika msitu huo na kujionea uharibifu mkubwa wa mazingira wa ukataji miti na uchomaji mkaa.
Mpogolo alisema baada ya kukamata magunia hayo serikali imeyataisha na baada ya kuyauza fedha hizo zitatumika kujengea maabara ya Shule ya Sekondari ya Ikungi.
Alisema kufuatia hatua hiyo mfanyabiashara aliyekamatwa na mkaa huo aliyetajwa kwa jina la Rose Nari kutoka mkoani Arusha kuwa atachukuliwa hatua za kisheria na wale maofisa wa TFS waliohusika katika tukio hilo watawasiliana na TFS makao makuu na mkoa kuona ni hatua gani watawachukulia na kwamba watalifuatilia suala hilo kwa karibu kuona mwisho wake.