Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, akifungua mafunzo ya Kamati za Ukaguzi za mafungu yote yaliyopo Makao Makuu ya Wizara ya fedha kuhusu Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani wa Wizara hiyo, yanayofanyika Mkoani Morogoro, ambapo amesisitiza usimamizi madhubuti wa fedha za umma.
Na. Peter Haule, WF, Morogoro
Wajumbe wa Kamati za Ukaguzi za Wizara ya Fedha wametakiwa kusimamia kikamilifu Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani wa Wizara (Internal Control Framework) ili kuboresha ufanisi wa utendaji na kufikia malengo ya Wizara yaliyokusudiwa.
Hayo yameelezwa Mkoani Morogoro na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya kamati za ukaguzi za mafungu yaliyopo makao makuu ya Wizara ya Fedha kuhusu Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani wa Wizara hiyo.
Alisema kuwa Wizara imeamua kuandaa Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani kwa kushirikiana na Mshauri elekezi ambaye ni kampuni ya KPMG ili kuwa na jicho la nje katika kuboresha taratibu za udhibiti wa fedha za umma.
“Serikali imetengeneza mifumo ya fedha ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato lakini kuna baadhi ya watu wanatengeneza mifumo ya pembeni wanayoitumia kuchepusha fedha za Serikali jambo ambalo halikubaliki”, alisema Bi. Omolo.
Bi. Omolo alisema kuwa kwa kuzingatia majukumu ya kamati za ukaguzi yaliyoainishwa katika kifungu cha 31 cha Sheria ya Fedha za Umma Sura 348 na kwa kuzingatia Mwongozo wa Serikali wa uandaaji wa mifumo ya Udhibiti wa Ndani ya Taasisi za umma wa mwaka 2014, Wizara imewasilisha rasimu ya Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani ili kupata maoni kutoka kwa wajumbe wa Kamati za Ukaguzi za Wizara kabla ya kuidhinishwa.
Alisema kuwa Mwongozo huo unalenga kutekeleza majukumu ya Wizara kwa kuzingatia maadili na taratibu zilizopo, kuongeza uwajibikaji na kusimamia vihatarishi vya Wizara.
Alisema wajibu wa Kamati za Ukaguzi wa Ndani wa Wizara ni pamoja na kuuelewa Mwongozo husika, maeneo ya mifumo ya Wizara yenye mchango mkubwa katika kufikia malengo yake, kupokea taarifa, kuzichambua na kutoa maoni na ushauri utakaowezesha kuboresha utendaji wa Wizara hiyo.
Aidha, Bi. Omolo ameishukuru kampuni ya ushauri elekezi ya KPMG kwa kushirikiana vyema na Wizara katika kuandaa Mwongozo huo wa Udhibiti wa Ndani na kwa kutoa mada za mafunzo na alitoa rai kwa wajumbe wa Kamati za Ukaguzi za Wizara kuendelea kukamilisha kazi hiyo kupitia mafunzo yanayotolewa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya Fungu namba moja (Vote 001) linalohusu Deni la Taifa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango TAMISEMI, Bw. John Cheyo, alisema kuwa Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani wa Wizara ya Fedha utarahisisha kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya na kujenga uelewa wa pamoja kwa Kamati zote za Ukaguzi za Wizara ya Fedha Makao Makuu.
Bw. Cheyo ameahidi kwa niaba ya Kamati za ukaguzi za Wizara kufanyia kazi Mwongozo huo na kuisaidia Wizara kufikia malengo yaliyokusudiwa na pia alishauri uandaaji wa Miongozo kama hiyo ifanyike kwenye Wizara zingine ili kurahisisha utendaji kazi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya Fungu Moja (Vote 001) linalohusika na usimamizi wa Deni la Taifa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango TAMISEMI, Bw. John Cheyo, akimshukuru Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo (katikati), kwa kuandaa Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani wa Wizara katika kuboresha ukaguzi wa ndani, wakati wa kufungua mafunzo kuhusu mwongozo huo yaliyofanyika Mkoani Morogoro. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani wa Wizara hiyo, Bw. Evarsto Mwalongo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya Fungu Moja (Vote 001) linalohusika na usimamizi wa Deni la Taifa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango TAMISEMI, Bw. John Cheyo, akimwongoza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, alipowasili kufungua Mafunzo ya Kamati za Ukaguzi za mafungu yote yaliyopo Makao Makuu ya Wizara ya Fedha kuhusu Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani wa Wizara hiyo, yanayofanyika Mkoani Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo (kushoto) na Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya Fungu Moja (Vote 001) linalohusika na usimamizi wa Deni la Taifa, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango TAMISEMI, Bw. John Cheyo, wakisikiliza kwa makini maelezo ya wajumbe wa Mafunzo ya Kamati za Ukaguzi za Mafungu yote yaliyopo Makao Makuu ya Wizara ya Fedha (hawapo pichani) kuhusu Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani wa Wizara hiyo, yanayofanyika Mkoani Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo (wa pili kulia, waliokaa) na Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya fungu Moja (Vote 001) linalohusika na usimamizi wa Deni la Taifa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango TAMISEMI, Bw. John Cheyo (kulia)wakiwa katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya maandalizi ya Mafunzo ya Kamati za Ukaguzi za mafungu yote yaliyopo Makao Makuu ya Wizara ya Fedha kuhusu Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani wa Wizara hiyo, yanayofanyika Mkoani Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo (wa pili kulia, waliokaa) na Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya Fungu Moja (Vote 001) linalohusika na usimamizi wa Deni la Taifa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango TAMISEMI, Bw. John Cheyo (kulia),wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa mafunzo hayo na wawezeshaji kutoka Kampuni ya KPMG walioshiriki kuandaa Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani wa Wizara hiyo, Mkoani Morogoro.
Mjumbe kutoka Kampuni ya KPMG, Bi. Peninah Musya, akitoa mada wakati wa Mafunzo ya Kamati za Ukaguzi za mafungu yote yaliyopo Makao Makuu ya Wizara ya Fedha kuhusu Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani wa Wizara ya Fedha, Mkoani Morogoro.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Morogoro)