Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akihimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Taasisi ya Uongozi (UONGOZI Institute) ( hawapo pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam jana.
Baadhi ya watumishi wa Taasisi ya Uongozi (UONGOZI Institute) wakisikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa kikao kazi cha watumishi hao na Naibu waziri huyo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kilichofanyika katika ukumbi wa Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Taasisi ya Uongozi (UONGOZI Institute) mara baada ya kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam jana.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Prof. Joseph Semboja akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) mara baada ya Naibu Waziri huyo kuwasili katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kikao kazi cha kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.
………………………..
Na. Aaron Mrikaria – Dar es Salaam
Serikali imeitaka Taasisi ya UONGOZI (UONGOZI Institute) kutoa mafunzo ya ungozi kwa viongozi mbalimbali wa Serikali katika maeneo yao kazi ili kuiwezesha Serikali kufikia lengo la kuimarisha utawala bora, badala ya kusubiri viongozi hao kufuata huduma mafunzo katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watendaji wa taasisi hiyo, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam jana kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, kuwapelekea mafunzo viongozi wa Serikali katika maeneo yao ya kazi kutapunguza gharama kubwa zinazotumika kuwasafirisha viongozi hao kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata semina elekezi na mafunzo mbalimbali ya uongozi yanayotolewa na taasisi hiyo.
Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa, mafunzo ya viongozi yakitolewa mahala pa kazi yatasaidia kuharakisha utoaji wa elimu ya maadili kwa viongozi wa umma, hivyo taasisi hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika kuwezesha kuifikia azma ya Serikali ya kuwa na viongozi waadilifu.
Sanjali na hilo, Dkt. Mwanjelwa ameitaka Taasisi ya UONGOZI kuhakikisha inatoa elimu ya umuhimu wa viongozi katika Taasisi zote Umma nchini kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Aidha, Dkt. Mwanjelwa ameishauri taasisi hiyo kuhakikisha inawasilisha Serikalini wazo lao la kuanzisha Kituo cha Tathmini ya Viongozi kwani kituo hicho kitakuwa ni msaada mkubwa kwa viongozi kutambua maeneo ambayo hawafanyi vizuri kiutendaji na kuyaboresha na kwa yale wanayofanya vizuri kiutendaji kuyaendeleza.
Naye, Mkuu wa Idara ya Mafunzo kwa Viongozi wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo amesema, Taasisi hiyo imeshatoa mafunzo elekezi kwa viongozi mbalimbali nchini kwa vipindi tofauti licha ya kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya viongozi kutomaliza mafunzo yao na wengine wanapomaliza hatua ya mwanzo hawaendelei na hatua inayofuata kwa mujibu wa taratibu ya mafunzo husika.
Pamoja na kuwepo kwa changamoto hiyo, Bw. Singo hakusita kuishauri Serikali kuendelea kuweka msisitizo wa kutoa mafunzo kwa viongozi wanaoteuliwa ili kuwajengea uwezo kiutendaji utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
“Taasisi ya UONGOZI inaishauri Serikali kuwa na utaratibu endelevu wa kutoa mafunzo kwa viongozi kabla ya kupandishwa vyeo, na iendelee kusisitiza utoaji wa mafunzo elekezi kwa viongozi wanaoteuliwa ili kuwajengea uelewa wa namna Serikali inavyofanya kazi, ikiwa ni pamoja na kuwapatia fursa ya kufahamu vipaumbele vya Serikali na miiko ya Utumishi wa Umma’’, Bw. Singo amesisitiza.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI Prof. Joseph Semboja amemshukuru Dkt. Mwanjelwa kwa kufanya ziara ya kikazi kuhimiza uwajibikaji katika Taasisi yake na kumhakikishia kuwa, taasisi yake itafanyia kazi maelekezo na ushauri alioutoa kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Taasisi hiyo.
Ziara hiyo ya kikazi ya Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) katika Taasisi ya UONGOZI ni mwendelezo wa utekelezaji wa majukumu yake ya kusimamia na kuhimiza uwajibikaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.