Na Muhidin Amri,
Mpanda
WANAFUNZI na walimu wa shule ya sekondari Machimboni wilaya ya Mpanda mkoani Katavi,wameishukuru serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa kuwafikishia mradi wa maji safi na salama.
Wamesema,mradi huo umewezesha kupungua kwa tatizo sugu la utoro na kuinua kiwango cha taaluma katika shule hiyo,kwa kuwa wanafunzi wanatumia muda mfupi kwenda kuchota maji kwa ajili ya kupikia,kufanya usafi wa mazingira na usafi wa mwili hivyo kuwawezesha kuwahi vipindi vya masomo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake Sabina Yegela alisema, katika shule hiyo kulikuwa na shida kubwa ya maji safi na salama,hali iliyohatarisha afya zao kutokana na kutumia maji ya visima vya asili ambayo hayakuwa safi na salama na kutembea umbali mrefu .
Yegela alisema,kabla ya mradi huo walikuwa wanatumia wastani wa Dk 40 hadi 60 kwenda kutafuta maji kwa matumizi ya shule hususani kwa ajili ya kupikia na usafi wa mazingira.
Alisema,hali hiyo iliwafanya kupoteza muda mwingi wa masomo kwenda kusaka maji badala ya kuwa darasani na walilazimika kufanya hivyo kwa sababu hawakuwa na njia mbadala ya kupata huduma ya maji ya uhakika na yaliyo safi na salama.
Aidha alisema,tofauti na mahitaji ya shule kuna wakati walilazimika kutembea umbali kati ya kilomita moja au mbili na wazazi wao kwenda na kurudi kuchota maji na hivyo kuathiri muda wa kujisomea wanaporudi nyumbani saa za jioni.
Aliongeza kuwa,walimu walipenda kutumia muda wanaotumia kwenda kuchota maji kufundisha watoto darasani,lakini mahitaji ya maji yaliwafanya kuvunja ratiba ya masomo ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana muda wote hapo shuleni kutokana na umuhimu wake.
Kaimu mkuu wa shule hiyo Martin Kahema alisema,ujio wa mradi huo wa maji umeleta manufaa makubwa hasa ikizingatia kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi wa shule hiyo wanaishi eneo la shule.
Alisema,mradi huo umewezesha kupata maji ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya shule na familia za walimu na kuishukuru serikali ya awamu ya sita kuwafikishia huduma ya maji.
Pia,amewapongeza wataalam wa Ruwasa kwa kutekeleza mradi huo na kuhaidi kuulinda kwa nguvu zote ili udumu kwa muda mrefu kwa kuwa hawakutegemea kama watapata maji safi na salama.
Kwa upande wake meneja wa Ruwasa wilaya ya Mpanda Mhadisi Christian Mpena alisema,mradi huo ulijengwa kwa njia ya mkandarasi kwa gharama ya Sh.milioni 265 na unahudumia jumla ya wananchi 3,200 wa kijiji cha Kapanda na taasisi za umma ikiwemo shule ya sekondari Machimboni na zahanati ya Kapanda.
Alisema,katika uendeshaji wa mradi Ruwasa imeunda chombo cha watumia maji kinachojulikana kwa jina Masi chenye jukumu ya kufanya matengenezo pindi unapoharibika na kukusanya fedha zinazotokana na mauzo ya maji kwa wananchi.