Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya, Dk Darison Andrew akizungumza jambo alipoongoza kikao cha tathmini ya Utekelezaji Mkataba wa Lishe cha robo ya kwanza ya Mwaka wa fedha 2023/24.
Wajumbe wakishiriki kikao cha tathmini ya Utekelezaji Mkataba wa Lishe cha robo ya kwanza ya Mwaka wa fedha 2023/24 katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya(Picha na Joachim Nyambo).
Na Joachim Nyambo, Chunya.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya imesema imejipanga kuhakikisha inaondoka nafasi ya tatu kitaifa na kushika nafasi ya kwanza kwenye utekelezaji wa Mkataba wa Lishe lengo likiwa ni kuwezesha wakazi wa wilaya hiyo kuwa na Afya bora.
Miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele kwenye utekelezaji wa Mkataba wa Lishe wilayani hapa ni pamoja na uimarishaji wa elimu ya Lishe bora kwa jamii juu ya mama wajawazito na watoto wachanga hususani kwa kuhakikisha wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita tangu kuzaliwa.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya, Dk Darison Andrew alibainisha hayo alipomwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Tamim Kambona kuongoza kikao cha tathmini ya Utekelezaji Mkataba wa Lishe cha robo ya kwanza ya Mwaka wa fedha 2023/24.
Dk Andrew alisema lengo la halmashauri ni kuona wakazi wilayani hapa wanaendelea na shughuli zao za kila siku zikiwemo za uzalishaji mali kwa kuepuka changamoto za kiafya zinazoweza kusababishwa na ukosefu wa lishe bora hivyo kuzitaka idara zote zilizo chini ya ofisi ya Mkurugenzi mtendajikujipanga kwa namna zote ili kufanikisha dhamira hiyo.
Alisisitiza pia kuwa elimu kwa jamii juu ya lishe bora hasa kwa wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ni muhimu kupewa nguvu kwakuwa ni sehemu ya njia za kuwashirikisha wananchi kutambua nini lengo la serikali mpaka ikaweka mkakati wa kuweka mkataba wa kusimamia jambo hilo.
“Matamanio yetu Halmashauri ya wilaya ya Chunya ni kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika utekelezaji wa mktaba wa Lishe. Hivyo lazima tujipange kuhakikisha tunatimiza azma hiyo na ili tuitimize lazima tushirikiane kwa pamoja kuanzia sisi mpaka mtu wa mwisho kabisa katika Mnyororo wa Lishe ambaye ni mwananchi.” Alisisitiza Dk Andrew.
“Wakati wataalamu tukijipanga kwa upande wetu kuutekeleza ni muhimu wananchi nao wakashirikishwa kwa karibu kutambua juhudi zinazofanywa na serikali yao kwenye kuimarisha afya zao kupitia lishe bora. Wananchi pia wawe washiriki wa karibu kwenye hili kwakuwa ndiyo walengwa.”
Mganga Mkuu huyo pia aliwataka maafisa Elimu Msingi na Sekondari kusimamia kwa karibu suala la upatikanaji wa chakula shuleni na kutawa wazazi na walezi wanaokwamisha jambo hilo kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwenye kikao hicho, Afisa Lishe wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya, Rehema Hiluka alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa namna ambavyo amekuwa akihakikisha fedha zote zilizopangwa kwaajili ya utekelezaji na usimamizi wa lishe zinatolewa kama bajeti inavyoelekeza huku akisema zimekuwa zikitolewa pia kwa wakati.
“Pamoja na kutoa taarifa za kikao cha tathimini ya mkataba wa lishe kitaifa wa robo iliyopita ambapo wilaya ya Chunya ilishika nafasi ya tatu kitaifa naomba kipekee nikushukuru Mkurugenzi kwa namna ambavyo anahakikisha fedha zilizopangwa kwaajili ya kutekeleza Mkataba wa Lishe zinatolewa na pia zinatolewa kwa wakati sahihi. Na kwa robo hii ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 tayari tumepokea fedha zaidi ya lengo yaani asilimia 126.” Alisema Hiluka.
Lengo la kufanyika kwa vikao vya Tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa kila robo ya mwaka wa fedha ni kuwezesha wadau kutambua mwenendo wake ili kuweza kubaini mafanikio na iwapo kuna changamoto zozote zinazobainika ziweze kutafutiwa ufumbuzi.
Wadau wa masuala ya kijamii wilayani hapa wanautaja Mkataba wa Lishe ambao Rais Samia Suluhu Hassan aliingia makubaliano ya utekelezaji na wakuu wa mikoa nchini na kisha wao kutiliana saini na wakuu wa wilaya kuwa miongoni mwa nyenzo muhimu zinazoimarisha Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kwenye eneo la Lishe Bora.
Baadhi ya wakazi wilayani hapa wakiwemo wajawazito wanaohudhuria huduma za Kliniki katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya wanasema msukumo wa utoaji elimu ya lishe bora unaonekana kuwa mkubwa katika siku za hivi karibuni.
Hata hivyo wanawake hao walikiri kuwepo bado na changamoto ya wanaume kutochangamkia juhudi hizo kutokana na kutoshirikiana na wake zao kufika kliniki hasa wakati wa ujauzito ili wapate elimu huku jamii za wafugaji na wachimbaji zikitajwa zaidi kwenye eneo hilo.