Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akitoa maelezo wakati akizindua Ufadhili wa masomo kwa Wanafunzi wa Kike wanaosoma Programu za Uhandisi katika sekta ya usafirishaji na kuweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa majengo matano ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) yanayojengwa kupitia Mradi wa Kujenga Ujuzi na Ushirikiano wa Kikanda wa Afrika Mashariki ( EASTRIP) unaofadhili na Benki ya Dunia .
………………………
Serikali imevitaka vyuo vya elimu ya juu na kati nchini kuandaa vijana kuwa na ujuzi kwa ajili ya kushiriki katika soko la ajira la ndani ya nchi na kimataifa.
Wito huo umetolewa Oktoba 28, 2023 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akizindua Ufadhili wa masomo kwa Wanafunzi wa Kike wanaosoma Programu za Uhandisi katika sekta ya usafirishaji na kuweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa majengo matano ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) yanayojengwa kupitia Mradi wa Kujenga Ujuzi na Ushirikiano wa Kikanda wa Afrika Mashariki ( EASTRIP) unaofadhili na Benki ya Dunia .
Prof. Mkenda amesema kuwa tatizo la ajira ni changamoto duniani kote, hivyo njia pekee ya kuwasaidia vijana kutoka katika changamoto hiyo ni kuhakikisha elimu inayotolewa inawaandaa na kuwawezesha kuwa mahiri ili kushiriki na kutafuta ajira popote duniani.
” Tatizo la ajira ni changamoto katika dunia kwa sasa, njia pekee ni kufundisha vijana wetu kuweza kutafuta fursa za ajira duniani na tusiwaandae kwa ajili ya soko la ajira la ndani tu, tunataka tukienda Congo, Malawi, Canada, Sweden kokote dunini tuwakute vijana wa kitanzania wanafanya kazi huko” amesisitiza Prof. Mkenda
Waziri Mkenda amesisitiza kuwa ni lazima elimu inayotolewa iwe na viwango vya kimataifa na kuwataka viongozi wa taasisi za elimu kuhakikisha zinapeleka wakufunzi wengi zaidi kupata uzoefu, maarifa na stadi kutoka duniani kote ili wanaporudi waweze kutoa mafunzo bora kwa vijana.
Aidha, ameongeza kuwa sasa umefika wakati wa vyuo kuanza kutoa zaidi Stashahada na kwamba katika kuhakikisha hili linafanikiwa serikali imeanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma stashahada ili kuongeza idadi ya vijana wenye ujuzi na stadi zinazohitajika katika soko la ajira.
“Stashahada ni muhimu sana , hapo nyuma zilipotea kwa kuwa hakukuwa na mikopo hivyo vyuo vyote vilibadilika na kuanza kutoa shahada , sasa habari njema ni kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Stashahada ili kuwezesha vyuo vingi zaidi kutoa programu za stashahada” amesema Prof. Mkenda.
Waziri huyo amekipongeza Chuo cha NIT kwa kutoa mafunzo ya masuala ya anga ikiwemo kozi za urubani ambapo amesema itasaidia katika kuwezesha vijana wa kitanzania kupata mafunzo hayo kwa gharama nafuu kwani mafunzo hayo yanatolewa kwa gharama kubwa katika nchi nyingine hivyo inakuwa ngumu kwa kijana anayetoka katika familia isiyokuwa na uwezo kupata mafunzo hayo hata kama ana uwezo wa akili.
Mhandisi Prof. Mganilwa ameongeza kuwa mbali ya kuanzishwa kwa kituo cha Umahiri pia kimeanza kutoa Ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa kike hasa wanaotoka katika mazingira magumu na wale wenye ufaulu wa juu katika masomo kuanzia ngazi ya stashahada hadi Uzamili.
Naye Mmoja wa wanufaika wa ufadhili huo Zawadi Kamote ameishukuru Serikali kupitia chuo hicho kwa kupata ufadhili huo na kwamba ataweka bidii ili kupata matokeo ambayo yatamwezesha kushiriki katika kujenga uchumi wa Taifa, huku akiwataka watoto wa kike kusoma kwa bidii kwani serikali inatoa fursa nyingi za kusaidia watoto wa kike kujiendeleza kiuchumi.