Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua bidhaa wakati akitembelea mabanda mbalimbali katika Maonesho ya Nne ya SIDO Kitaifa yanayofanyika uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe.
………………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Taasisi za fedha nchini kuweka masharti ya mikopo ya upendeleo kwa Viwanda vidogo na vya kati ili kukuza uzalishaji na kuimarisha sekta hiyo.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa kilele cha Maonesho ya Nne ya Kitaifa ya Shirika la Kuhudumiwa Viwanda Vidogo (SIDO) yaliyofanyika katika uwanja wa sabasaba mkoani Njombe. Amesema ni muhimu kushughulikia suala la upatikanaji wa mitaji kwa riba nafuu ili kuwawezesha wajasiriamali kuweza kuanzisha viwanda vidogo na vya kati.
Aidha Makamu wa Rais amesema Katika kuongeza thamani ya bidhaa na mazao, suala la vifungashio lina umuhimu mkubwa hivyo SIDO na taasisi nyingine katika tasnia ya Viwanda vidogo vidogo inayo nafasi ya kutoa mchango katika kubuni na kuhamasisha uzalishaji wa vifungashio bora na vyenye viwango kwa kutumia teknolojia rahisi na nafuu. Pia amesema tafiti zina umuhimu mkubwa katika kukuza matumizi ya teknolojia mbalimbali kwenye uzalishaji na uongezaji thamani wa bidhaa na mazao.
Makamu wa Rais ameitaka SIDO kuanza kujiendesha kibiashara pamoja na kuanzisha tuzo kwa wabunifu wa mashine na wazalishaji bora wa bidhaa kutoka viwanda vidogo vidogo katika mfumo wa fedha, vyeti au mafunzo maalum kwa wajasiriamali waliofanya vizuri zaidi. Pia ameagiza shirika la viwango (TBS) kufanya jitihada zaidi kuwafikia wajasiriamali wadogo kupata uthibitisho wa ubora wa bidhaa zao kwa gharama nafuu.
Makamu wa Rais amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kujenga uchumi shindani wa viwanda ili kuifikisha nchi kwenye kipato cha kati cha juu. Amesema maonesho hayo yamesaidia kuibua masuala kadhaa yanayoathiri maendeleo ya viwanda vidogo vidogo.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amesema Serikali imedhamiria kujenga uwanja mpya wa ndege wenye urefu wa kilomita tatu utakaowezesha ndege kubwa za abiria na mizigo kutua pamoja na ujenzi wa jengo la abiria na jengo maalum la kuhifadhia bidhaa zinazoharibika haraka (cold room) katika mkoa wa Njombe. Pia amesema Wizara ya Elimu inatambua umuhimu wa ujenzi wa Chuo Kikuu katika mkoa huo na kwa hatua za awali taratibu za kuanzisha Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) zinaendelea kufanyika na zitakapokamilika ujenzi utaanza mara moja.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amesema Wizara hiyo inaendelea kupitia na kufanya marejeo ya sera na sheria mbalimbali za taasisi ikiwemo sheria iliyounda SIDO ili kuendana na hali ya sasa ambayo italiwezesha shirika hilo kutoa huduma zenye tija na ushindani.
Ameongeza kwamba serikali imewezesha upatikanaji wa fedha ambazo zimesaidia SIDO kuboresha miundombinu yake ikiwemo kuboresha vituo sita vya uendelezaji wa teknolojia na ubunifu kwa kuweka mitambo ya kisasa yenye thamani ya shilingi bilioni 1.65 katika mikoa ya Mbeya, Kilimanjaro, Iringa, Shinyanga , Lindi na Kigoma. Pia kuongeza mtaji wa shilingi bilioni 1.69 kwenye mfuko wa kukopesha wajasiriamali (NEDF).
Awali akitoa taarifa za maonesho hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Sido Mhandisi Mussa Nyamsingwa amesema maonesho hayo yanalenga kuwawezesha wananchi kufahamu huduma zinazotolewa na SIDO na bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla. Aidha amesema maonesho hayo yamekuwa yakichochea ukuaji wa ajira, kutekeleza shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali hasa katika uongezaji wa thamani wa mazao pamoja na kuchochea ubunifu na uzalishaji wenye tija.
Maonesho hayo yenye kauli mbiu isemayo “Pamoja Tujenge Viwanda Kwa Uchumi na Ajira Endelevu” yalianza tarehe 21/10/2023 ambapo yameshirikisha wajasiriamali wapatao 805, Teknolojia 95 zinazotumika katika Minyororo 22 ya thamani ya mazao na Taasisi 30 za Serikali na Binafsi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na viongozi mbalimbali wakati akiwasili katika uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe kushiriki kilele cha Maonesho ya Nne Kitaifa ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Prof. Silvester Mpanduji wakati alipotembelea banda la SIDO katika Maonesho ya Nne ya SIDO Kitaifa yanayofanyika uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua bidhaa wakati akitembelea mabanda mbalimbali katika Maonesho ya Nne ya SIDO Kitaifa yanayofanyika uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akitembelea mabanda mbalimbali katika Maonesho ya Nne ya SIDO Kitaifa yanayofanyika uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimpongeza mbunifu wa kinu cha kufua chuma Bw. Reuben Mtitu wakati alipotembelea banda la mbunifu huyo katika Maonesho ya Nne ya SIDO Kitaifa yanayofanyika uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa kilele cha Maonesho ya Nne ya SIDO Kitaifa katika uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe.