Afisa lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya ndugu Simon Mayala akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya Lishe kwa wanafunzi hasa Rika Balehe, Hapo ni shule ya Sekondari Kiwanja
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Itewe wakiwa katika utulivu wakati wakipewa elimu ya Lishe na Maafisa toka ofisi za elimu, na wataalamu wa lishe.
Na Joachim Nyambo, Chunya.
WAKAZI wilayani Chunya mkoani Mbeya wamepongeza hatua ya serikali kuendesha Kampeni ya Lishe vijana balehe yenye lengo la kutoa elimu ya lishe kwa vijana na namna bora ya ulaji unaozingatia afya.
Wakazi hao wamesema serikali imechukua hatua nzuri kuwa na mpango wa kutoa elimu ya lishe kwa vijana balehe wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari kwakuwa haitoishia kuwawezesha wao pekee kuimarisha afya zao bali jamii inayowazunguka.
Mkazi wa Kijiji cha Nkwangu kilichopo Kata ya Upendo, Dionese Mamboleo alisema wanaiona kampeni hiyo kuwa na umuhimu zaidi kwakuwa vijana balehe wapo pia kwenye rika la kukaribia kuingia kwenye majukumu ya familia hivyo ni muhimu wakatambua umuhimu wa lishe bora.
Mamboleo alisema vijana balehe wakitambua lishe bora ni dhahiri kuwa watakuja kuwa walezi bora wa familia zao kwa kuzingatia mambo muhimu ikiwemo namna wajawazito na watoto wachanga wanavyopaswa kulishwa ili kuwawezesha kuwa na afya imara.
Mkazi wa mji mdogo wa Makongolosi, Tumaini Nelson au Mama Tina alisema kampeni ya lishe kwa vijana balehe inawajengea msingi vijana kuja kuwa mama na baba bora kwa familia zao watakapoingia kwenye ndoa na watazingatia kanuni za kuondokana na udumavu na utapiamlo kwa watoto wao kwakuwa watazingatia makundi ya vyakula kwa wajawazito na watoto watakaozaliwa.
Akiwa katika mikusanyiko ya Kampeni ya Kampeni ya lishe vijana balehe, ofisa lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Simon Mayala aliwataka wanafunzi na wanachunya kwa ujumla kubadili namna ya ulaji wa vyakula ili kuepukana na changamoto mbalimbali zinazotokana na ulaji mbaya.
Mayala alisisitiza umuhimu wa kuzingatia lishe bora huku akisema lishe bora ni kupata mlo kamili na sio kushiba kama ilivyozoeleka kwa jamii nyingi ikiwepo wanafunzi ambao baadaye ndio Taifa la kesho.
Miongoni mwa maeneo aliyosisitiza jambo hilo ni alipozungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kiwanja na Shule ya Sekondari ya kata ya Itewe ambapo aliwataka kutambua naamna nzuri ya ulaji.
“Lishe bora inaanza na namna ya ulaji…siyo kula na kushiba, hivyo vijana kama taifa la kesho tunapaswa kuzingatia namna ya ulaji bora kutokana na changamoto mbalimbali za kiafya zinazotokana na ulaji mbaya kwani kumekuwa na wimbi kubwa la magonjwa ya moyo hii yote ni kutokana na vyakula tunavyo vitumia” alisema Mayala
Mayala aliongeza kuwa vijana wanapaswa kula kwa kuzingatia afya jambo ambalo litasaidia kupunguza changamoto mbalimbali za kiafya kwa kutumia vyakula vinavyolinda mwili na kuwataka kuacha mara moja kula vyakula ambavyo vitawasababishia madhara ya kiafya kwa baadaye.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekodari ya Kiwanja, Jackson Mnyalape alisema elimu ya lishe wanoyoipata wanafunzi ni muhimu kwa maisha yao ya sasa na hata maisha yao ya baadaye kwani itawasaidia hata watakapokuwa na familia zao.
“Tunaweza kusema huu ni uwekezaji mkubwa na wenye faida kwa sasa na baadaye. Vijana hawa ndiyo wanaotegemewa kuja kuwa wazazi na walezi. Sasa taifa letu liko katika mjdadala wa kuhakikisha uwekezaji kwa watoto kuanzia miaka sifuri hadi minane unapewa msukumo. Lishe ni sehemu ya uwekezaji huo hivyo wanapofundishwa hawa tunawekeza pia watu wa kuja kusaidia usimamizi wa lishe bora kwa jamii.” alisema
Kwa upande wao wanafunzi Dorah Daniel na Isack Sajire kutoka sekondari ya Kiwanja na Norberth Mawazo na Anastazia Ndede sekondari Itewe walisema elimu ya lishe waliyoipata itawasaidia kupunguza au kuacha kula vyakula ambavyo vitawasababishia changomoto za kiafya kwa baadaye.
Walisema pia upimaji wa hali ya lishe waliofanyiwa kupitia kampeni hiyo umewasaidia kujua hali zao za lishe na kujua wanatakiwa kufanya nini ili kuboresha zaidi hali zao za lishe na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa masuala ya lishe hata watakaporudi majumbani kwao.
Kampeni ya lishe vijana balehe yenye kauli mbiu ‘Lishe kwa Vijana Balehe , Chachu ya Mafanikio yao’ ilianza Oktoba 16 mwaka huu ambapo kwa wilayani Chunya imezifikia Shule za Sekondari Isenyela, Kiwanja na Itewe ambapo wanafunzi 756 wamepima hali zao za Lishe wakati wa Kampeni hiyo.
Utekelezaji wa kampeni hiyo ulijumuisha wataalamu mbalimbali wakiwemo Maafisa elimu Sekondari wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya, Wauguzi kutoka hospitali ya Wilaya ,walimu pamoja na Wanafunzi.
Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) inaitaja Lishe bora kuwa miongoni mwa maeneo makuu matano yanayopaswa kuzingatiwa kwenye ukuaji wa awali wa mtoto hiyo kwa vijana balehe kujengewa msingi wa elimu ya ulaji sahihi ni mwelekeo mzuri wa wao kuja kuwa walezi wazuri wa watoto wao watakapoingia kwenye ndoa.