Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe,akizungumza katika Kikao kilichokutanisha Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Bandari(TPA) na wakulima pamoja na wasafirishaji wa mboga mboga jijini Dodoma
Mdau kutoka TAHA,Bi. Jacqueline Mkindi,akitoa taarifa kwenye Kikao kilichokutanisha Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Bandari(TPA) na wakulima pamoja na wasafirishaji wa mboga mboga jijini Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James,akitoa ufafanuzi katika Kikao kilichokutanisha Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Bandari(TPA) na wakulima pamoja na wasafirishaji wa mboga mboga jijini Dodoma.
Sehemu ya wabunge wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji pamoja na wadau wakimsikiliza Mdau kutoka TAHA,Bi. Jacqueline Mkindi,akitoa taarifa kwenye Kikao kilichokutanisha Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Bandari(TPA) na wakulima pamoja na wasafirishaji wa mboga mboga jijini Dodoma.
Afisa Mkuu wa Utafiti wa Masoko,Bi.Lydia Mallya,akitoa taarifa kwenye Kikao kilichokutanisha Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Bandari(TPA) na wakulima pamoja na wasafirishaji wa mboga mboga jijini Dodoma
………………..
Na Alex Sonna,Dodoma
SERIKALI imekutana na wakulima na wasafirishaji wa mboga mboga kuangalia changamoto za kodi na kisera ili kuweka mipango ya miaka mitatu ijayo ikiwemo chombo kitakachosimamia sekta hiyo.
Akizungumza kuhusu kikao kilichokutanisha Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Bandari(TPA) na wakulima hao, Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, amesema kikao hicho kinalenga kuangalia changamoto hizo ili kutengeneza muelekeo wa miaka mitatu ijayo.
“Tumekutana na wadau mbalimbali hawa wa kilimo cha mboga mboga wameeleza changamoto zao kwa uwazi na tumekubaliana kuwa na timu ndogo ambayo itatengeneza mapendekezo ndani ya mwezi mmoja ili yaweze kufanyiwa kazi na serikali,”amesema.
Bashe amesema njia ya kushirikiana itasaidia kuondoa matatizo ya sekta ya kilimo.
“Kwa mfano wanasema kupitisha kontena kwa bandari ya Dar es salaam inachukua siku 10, sasa kontena la parachichi ukaliweka kwenye mstari mmoja na copper likikaa siku 10 litaharibika ndio maana wengi wanapitishia bandari ya Mombasa ,”amesema.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri Bashe amesema TPA wamekubaliana kuweka mfumo ambao ni maalum kwa ajili ya kupitisha mazao ya kilimo na hayataingia kwenye msongamano wa makontena mengine.
“TPA wametuahidi wanaanzisha kitengo maalum kitakachohusisha TPA, TRA kuhakikisha mchakato wa kusafirisha makontena ya mazao ya kilimo haupitii mchakato mrefu, pia wamezungumzia kuhusu kodi kwenye vifungashio tunaamini baada ya mwezi huo mmoja wakileta ripoti tutaweka sawa road map yetu kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mitano ya sekta hii,”amesema.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa, amesema sekta ya kilimo ni uti wa mgongo na kwamba matokeo ya sekta ya mboga mboga ni makubwa, na kuishauri serikali kushughulikia changamoto zilizobainishwa ikiwemo utitiri wa tozo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, amesema wapo wawekezaji wa sekta hiyo walipewa fedha za mikopo lakini hadi sasa wengine wamekwama kurejesha na hakuna kilichofanyika.
“Tunahisi kuna watu walichukua fedha wakaenda kufanya miradi mingine lakini sio iliyokuwepo kwenye maandiko, maana tumeenda kuangalia kilichofanyika hakiendani kuna wengine tumechukua mashamba mmoja ameshindwa kulipa Sh.Bilioni 36 za serikali,”amesema.
Awali, Mdau kutoka TAHA, Jacqueline Mkindi, amesema kuna changamoto kwenye usafirishaji ili kufikia kwenye masoko ya mboga mboga.
“Kwa mfano hatuna ndege za mizigo tunategemea kutumia viwanja vya ndege vya nchi jirani, tunasafirisha kwa kutumia meli lakini tunatumia bandari ya Mombasa, hivyo vikwazo viondolewe ili kutumia bandari ya ndani na kuondoa changamoto na kupunguza gharama za usafirishaji,”amesema.