Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine akizungumza katika kikao na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi kuhusu mifuko mbadala aina ya ‘non-woven’ isiyokidhi viwango ambayo imebuka na kutumika kinyume cha sheria.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akitoa ufafanuzi kuhusu mifuko mbadala aina ya ‘non-woven’ isiyokidhi viwango.
Sehemu ya wajumbe wa Kikosi kazi cha Katazo la mifuko ya plastiki wakiwa katika kikao na waandishi wa habari.
Mratibu wa Mazingira kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI ambaye pia ni mjumbe wa Kikosi kazi cha kitaifa cha katazo la mifuko ya plastiki, Sanford Kway akifafanua jambo katika kikao hicho.
……………………….
Serikali imeanza msako wa kuwabaini waingizaji na wazalishaji wa mifuko mbadala aina ya ‘non woven’ isiyokidhi viwango vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) vya chini ya GSM 70.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ambapo alisisitiza kuwa mifuko inayotakiwa lazima iwe na jina la mzalishaji, uzito na mawasiliano ya mzalishaji.
Sokoine alisema kuwa kumezuka wimbi la mifuko isiyokidhi viwango vilivyowekwa hivyo matokeo yake wale ambao wameitikia wito wa kufungua viwanda vya mifuko mbadala wanakosa soko.
“Elimu kwa umma itaendelea kutolewa ili watu wajue mifuko ipi hairuhusiwi kutumika na hii itasaidia wazalishaji wa mifuko inayokidhi viwango kupata masoko na kuweza kuisambaza hadi kule kwenye changomoto na bei itakuwa ya kawaida ili kila mtu aweze kununua,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka alisema kuwa zoezi la katazo la mifuko ya plastiki kupitia Kikosi kazi cha Taifa limefanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Dkt. Gwamaka alisema kuwa kuanza sasa vifungashio vya plastiki vya katoni za maji havitaruhusiwa na kuwa badala yake yatumike maboksi kwani yanaweza kurejelezwa hivyo ni rafiki wa mazingir huku akiongeza kuwa magazeti hayaruhusiwi kufungashia bidhaa zikiwemo vyakula kama nyama kwani ni hatari kwa afya zikiwemo magonjwa ya kansa
Alisema kwa sasa mifuko hiyo imeondolewa lakini bado kuna changamoto ya vifungashio kugeuzwa vibebeo huku akionya viwanda vya vinavyojihusisha na uzalishaji wake.
“TBS imeshatoa kanuni za namna gani mifuko mbadala inayozalishwa lakini bado tunaona mifuko hii inazalishwa kwa wingi na tunajua bayana lazima mifuko hii iwe na GSM 70 ili kuwalinda lakini wale tunaowalinda wanazalisha usiku wanapeleleka sokoni sasa Serikali haijalala tumeanza msako wa kuwabaini na tutawachukulia hatua,” alionya.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema kuwa tayari kikosi kazi hicho kimekamata kiwanda kinachozalisha mifuko hiyo kilichopo jijini Dar es Salaam na kupiga faini huku akitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona viwanda kama hivyo na kuwa itatolewa zawadi kwao.