Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwasilisha Taarifa kuhusu Tathmini za Mazingira Kimkakati pamoja na ufanisi wa Tathmini za Athari kwa Mazingira (TAM) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira leo Oktoba 26, 2023 jijini Dodoma.
………………………
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema jumla ya vyeti 190 vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira vimetolewa kwa ajili ya miradi mbalimbali katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2023.
Amesema hayo wakati akiwasilisha Taarifa kuhusu Tathmini za Mazingira Kimkakati pamoja na ufanisi wa Tathmini za Athari kwa Mazingira (TAM) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.
Amesema hatua hiyo inaunga mkono azma ya Serikali kuelekea uchumi wa viwanda hivyo Ofisi imeendelea kupokea miradi mingi kutokana na ongezeko la wawekezaji katika mbalimbali.
Mhe. Khamis amesema pia Ofisi imechukua hatua mbalimbali na kuweka mipango ya utekelezaji kwa kupunguza muda wa mchakato wa TAM ambapo miradi hii huhitaji kupata cheti kilichosainiwa na Waziri mwenye dhamana ya Mazingira.
’’Kwa muongozo huu wa kanuni mpya kwa miradi yenye ulazima wa kupitia tathmini ya athari kwa mazingira muda umepungua na kufikia siku 95 kutoka 149 kama ilivyokuwa awali,’’ amesema Naibu Waziri Khamis.
Hali kadhalika Naibu Waziri amesema kwa kuzingatia umuhimu wake Miradi ya kimkakati ya Serikali ikiwemo viwanda na miradi ya kipaumbele ya kilimo inahusika katika vibali hivyo ambacho kinadumu kwa miezi minne ili kuruhusu mchakato wa TAM kwa mradi husika kukamilika na kupatiwa cheti.
Aidha, ameongeza kuwa Kupunguza Ada na Tozo za TAM, Kanuni za Ada na Tozo zimeboreshwa mwaka 2019 na mwaka 2021 ili kupunguza gharama za mapitio ya TAM.
“Ili kuleta maendeleo endelevu, suala la uhifadhi wa mazingira halina budi kupewa kipaumbele na ili kuhakikisha ufanisi wa miradi ni vyema kuhuisha masuala ya mazingira katika shughuli za maendeleo hususan ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira,” amesema.
Hivyo, Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea na jitihada katika kufanya mapitio ya Kanuni pamoja na miongozo mbalimbali ili kuboresha tathmini za athari kwa mazingira ikiwemo zile za kisekta ili kuhakikisha tunakidhi azma ya Serikali ya uchumi wa wiwanda ambao ni endelevu.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwasilisha Taarifa kuhusu Tathmini za Mazingira Kimkakati pamoja na ufanisi wa Tathmini za Athari kwa Mazingira (TAM) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira leo Oktoba 26, 2023 jijini Dodoma.
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwa katika kikao cha kuwasilisha Taarifa kuhusu Tathmini za Mazingira Kimkakati pamoja na ufanisi wa Tathmini za Athari kwa Mazingira (TAM) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira leo Oktoba 26, 2023 jijini Dodoma.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)