Na Elinipa Lupembe – Arusha
Kufuatia mkakati wa Serikali ya awamu ya sita wa kuongeza idadi ya shule za sekondari nchini ili kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata fursa ya kusoma darasa la kwanza mpaka kidato cha nne, hili limefanyika kwa vitendo kijiji cha Laja wilaya ya Karatu.
Hali ilikuwa tofauti kwa watoto wa kata ya Laja licha ya kuwa walipangiwa kujiunga na elimu ya sekondari kijiji jirani lakini wengi walikatisha masomo kutokana na umbali huku watoto wa kike wakibebeshwa mimba na wengine kuangukia kwenye ndoa za utotoni.
Wananchi wa Laja wameweka wazi kuwa, ujenzi wa shule mpya ya sekondari Laja utawapa furasa watoto wao kumaliza masomo yao kwa utulivu na itakuwa mkombozi kwa watoto wa kike kuondokana na mimba na ndoa za utotoni.
Christina Samson mkazi wa Laja amebainisha kuwa awali watoto wao walitembea umbali wa kuanzia Kilomita 5 mpaka 12 kwenda shule ya sekondari Karisan, jambo ambalo lilisababisha watoto kukatisha masomo huku wasichana wakirubuniwa na kubebashwa mimba jambo lililowalazimu kuacha masomo na wengine kuolewa katika umri mdogo.
Amesema kuwa baadhi ya wasichana walirubuniwa na madereva wa pikipiki na kujikuta wakiingia kwenye mtego na kubebeshwa mimba, kwa kuwa wazazi wengi walishindwa kulipia ada za hosteli ili watoto waishi shuleni kutokana na uwezo mdogo wa kifedha.
“Tunamshukuru mama Samia kwa kutujengea shule ya sekondari, shule hii ni mkombozi kwa watoto wetu, itatufuta machozi kina mama kwa kuwa watoto wetu sasa watasoma karibu na nyumbani, tunaamini watamaliza masomo salama kwa kuwa itatuwia rahisi wazazi kufuatilia maendeleo yao wakati wote wakiwa shuleni, kule mbali wengi tulishindwa” Amesema Christina
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Laja, Mhe. Samweli Yona Panga licha ya kumshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka, amebainisha kuwa Laja ilikuwa imesahaulika miaka mingi, ujenzi wa shule hii utawasaidia watoto wetu kusoma kwa amani na furaha wakiwa karibu na nyumbani.
“Laja tulitengwa lakini kwa huruma za mama, tumekumbukwa, tumepokea miradi mingi ya shule, barabara, zahanati, tunaendelee kumuunga mkono Rais wetu, tunamuombea afya njema” Amesema Mwenyekiti Panga.
Shule ya sekondari Laja imejengwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kwa gharama ya shilingi milioni 333.1