OR-TAMISEMI, ARUSHA
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amemuagiza Afisa Elimu Mkoa wa Arusha kuharakisha usajili wa Shule tarajiwa ya Msingi Lucas Mhina ili ipokee wanafunzi kwa ajili ya mwaka wa masomo 2024.
Mhe Ndejembi ametoa agizo hilo kwenye uzinduzi wa Shule hiyo katika Kijiji cha Losirwa wilayani Monduli mkoani Arusha.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mhe. Ndejembi amemuagiza pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Monduli kupeleka walimu wa kuanzia kwenye shule hiyo.
“Nimpongeze sana ndugu Lucas Mhina kwa uzalendo wake wa kuweza kutafuta wafadhili ambao wamejenga shule hii nzuri kwa ajili ya kusaidia jamii ya wafugaji kuweza kupata elimu lakini pia kusaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwani sasa shule imeletwa karibu.”
“Kama Serikali tunaunga mkono juhudi hizi hivyo nimuagize Afisa Elimu Mkoa kuhakikisha anaharakisha shule hii iweze kupata usajili ili iweze kuanza kupokea wanafunzi watakaojiunga Januari 2024 na
Mkurugenzi wa Halmashauri aangalie ikama yake ya walimu na alete walimu ambao wataanzisha shule hii huku pia sisi kama Serikali tukiangalia mchakato wa kuleta walimu zaidi hapa,” amesema Ndejembi.
Mhe Naibu Waziri Ndejembi ametoa rai pia kwa wananchi wa kijiji hiko cha Losirwa kuhakikisha wanalinda na kutunza miundombinu ya shule hiyo ili kuleta tija kwa wanafunzi watakaoanza masomo hapo.
Kwa upande wake, Mfadhili wa shule hiyo, Lucas Mhina amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoifungua Nchi kiuchumi na hivyo kuwawezesha wahisani mbalimbali kuja nchini kuwekeza na kusaidia miradi ya maendeleo huku akiahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuwaletea watanzania maendeleo.
Mhina ameikabidhi shule hiyo kwa Serikali ambapo tayari vyumba 20 vya madarasa , Ofisi ya Walimu, matundu 14 ya vyoo vya wanafunzi, matundu manne ya vyoo vya walimu, nyumba mbili za walimu zimejengwa pamoja na kuwekwa madawati 100, matanki mawili ya maji pamoja na kisima cha maji.