Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Makame Khatib Makame akifungua kikao cha kujadili utekelezaji wa Mpango wa kutokomeza Kipindupindu Zanzibar (ZACCEP) huko katika Ukumbi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Maruhubi .
Mkuu wa Kitengo, Mipango Utawala na Rasilimali Watu Haji Faki Hamdani akiuliza suala kwa Afisa wa Mamlaka ya Maji (ZAWA) katika kikao cha kujadili utekelezaji wa Mpango wa kutokomeza Kipindupindu Zanzibar (ZACCEP) huko katika Ukumbi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Maruhubi .
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati Utekelezaji wa Mpango wa Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar kutoka katika Taasisi mbali mbali wakisikiliza maelezo mafupi ya utekelezaji kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Makame Khatib Makame ( hayupo pichani) huko katika Ukumbi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Maruhubi .
…………………
Na Khadija Khamis Maelezo Zanzibar
Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Makame Khatib Makame amezitaka Taasisi mbali mbali zilizojumuishwa katika mpango wa kutokomeza Kipindupindu Zanzibar (ZACCEP) kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kufikia azma ya Serikali ya kuondoa kipindupindu Zanzibar .
Alisema mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika sekta mbali mbali za Serikali ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unaimarishwa kwa kudhibiti mazingira hatarishi na kutoa elimu kwa jamii ikiwemo watoto wa skuli .
Hayo aliyasema huko katika ukumbi wa kamisheni ya kukabiliana na maafa maruhubi wakati akifungua kikao cha utekelezaji wa mpango wa kutokomeza kipindupindu Zanzibar .
Alisema kila taasisi ifanye kazi kwa mujibu wa mujibu wa mpango huo ili iweze kurekebisha hali halisi ya mazingira ya mji na vijiji pamoja na kuweka mipango mikakati ya utekelezaji wa majukumu hayo.
Aidha alizitaka Taasisi husika ambazo zimo katika mpango wa kutokomeza kipindupindu kutoa elimu endelevu kupitia vyombo mbali mbali vya habari ili jamii iweze kujilinda na uchafu wa mazingira ambao hupelekea kupata maradhi ya mripuko.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo alizitaja hatua ambazo kamisheni itazichukuwa kwa kufanya ziara katika maeneo mbali mbali ya Mikoa yote ya Zanzibar ili kuona hali halisi ya utekelezaji wa mpango kwa Taasisi husika.
Nae muakilishi wa shirika la kuhudumia watoto ulimwenguni (UNICEF)Zanzibar Marko Msambezi alisema ataendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza mpango wa kutokomeza kipindupindu Zanzibar .
Alieleza kuwa ataendelea kutekeleza majukumu ya kazi kwa lengo la kuisaidia jamii pamoja na kuimarisha mazingira ili kuweza kuleta ufanisi
Muakilishi huyo alisema tayari ameshakamilisha ujenga wa vyoo katika maskuli mbali mbali ya msingi na kuhakikisha vyoo vilivyopo vinakwenda sambamba na idadi ya wanafunzi pamoja na kuahidi kuweka mifereji katika skuli zote ili kuwawezesha wanafunzi kusafisha mikono yao mara kwa mara .
Pia aliwataka wajumbe hao kuweza kuwasilisha taarifa zao za utekelezaji wa majukumu kwa kila taasisi husika kwa kila robo kota ili kuweza kujua utekelezaji mzima wa uratibu wa kipindupindu.
Nao Wajumbe wa Mpango huo walisema wanaendeleza na utekelezaji wa mpango wa kutokomeza Kipindupindu Zanzibar (ZACCEP) Kwa mashirikiano baina ya wizara tofauti ikiwemo afya mazingira manispaa, elimu, maji, halmashauri mbali mbali ili kuhakikisha usalama wa wananchi unapatikana kwa kuweza kukagua vianzio vya maji na kuweza kuyatibu maji na kutoa elimu ya utumiaji wa dawa za kutibu maji kwa wananchi.
Hata hivyo walieleza kuwa kuna baadhi ya maeneo ya mjini na vijijini kumebainika kukosekana kwa mashimo ya maji machafu jambo ambalo linachangia uchafuzi wa mazingira .
Walisema kuwa kumezuka utitiri wa uchimbaji holela wa visima katika maeneo mbali mbali ya mijini, visima ambavyo havina uhakika wa usalama wa maji licha ya kutolewa elimu ya utumiaji wa dawa kwa wananchi.
Kwa upande wa wajumbe kutoka Pemba walilalamikia changamoto ya ukosefu wa maji katika Mkoa wa Kusini Pemba walisema visima vingi vimekauka maji jambo ambalo huchangia uchafu wa mazingira katika baadhi ya vituo vya afya.
Wajumbe wa utekelezaji wa mpango huo walisema wameweza kupiga hatua ya utekelezaji kwa kuunda kikosi kazi cha ukaguzi wa mazingira na kusafisha mitaro na kuzoaji taka katika maeneo mbali mbali ukaguzi wa wafanyabiashara pamoja na sehemu ya biashara zao mabekari ya mikate na kadhalika ili kuhakikisha mpango unatekelezwa .