Ferdinand Shayo ,Manyara.
Kampuni ya Mati Super Brands Limited inayozalisha vinywaji changamshi imeshiriki maonyesho ya wiki ya vijana Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani wilayani Babati mkoani Manyara ambapo mamia ya vijana kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania wamepata fursa ya kuonyesha shughuli zao za kijasiriamali na kujifunza masuala mbali mbali ya biashara .
Akizungumza katika banda la kampuni hiyo,Afisa Masoko wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited Gwandumi mpoma amesema kuwa maonyesho hayo yamewapa fursa ya kukutana na wateja wao pamoja na wateja wapya ambao wameonyesha kuvutiwa na bidhaa bora zinazozalishwa na kampuni hiyo.
Mpoma amesema maonyesho hayo yanayapa fursa kubwa vijana kujifunza masuala mbali mbali ya ujasiriamali pamoja na namna ya kuanzisha biashara na kuziendeleza.
“Sisi kama Mati Super Brands Limited tunayo furaha kubwa kushiriki katika Maonyesho ya wiki ya vijana ambayo yamefana na tunatarajia yatakua na matokeo chanya” Anaeleza Mpoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ,SERA,Bunge na Uratibu Jenista Mhagama ametembelea banda la Mati Super Brands Limited na kuwataka waendelee kufanya miradi ya kuwawezesha vijana kiuchumi kama njia mojawapo ya kurejesha kwenye jamii sehemu ya faida wanayoipata.
“Ni vyema mkafanya mradi mmoja wa kuwawezesha vijana ambao utakua mfano kwa mkoa wa Manyara kama muendelezo wa shughuli za kusaidia jamii inayowazunguka hususan vijana” Anaeleza Waziri Mhagama