Kikosi kazi kilichoundwa na mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olesendeka kikiongozwa na kamanda wa polisi mkoa Hamis Issa kwa ajili ya kufatilia madeni kwa wadaiwa sugu waliopelekea benki ya wananchi Njombe NJOCOBA kuingia mufilisi kimefanikiwa kukusanya zaidi ya mil 300 kati ya bil 1.5 ambazo zipo kwenye mikono ya watu.
Jan,2018 benki ya wananchi NJOCOBA iliingia mufilisi baada ya kushindwa kujiendesha kutokana na madeni hayo jambo ambalo liliibua malalamiko kwa wateja ambao waliweka fedha na kushindwa kuzitoa wanapohitaji kutoa.
Kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa mezani kwa mkuu wa mkoa imeonyesha watu 71 kati 336 wamefanikiwa kurejesha fedha na kumaliza madeni yao huku wadaiwa 216 wakiwa hawajalipa kiasi chochote na kushindwa kutoa taarifa mahala popote.
Akizungumza na vyombo vya habari kuhusu hatua iliyofikiwa katika zoezi hilo Christopher Olesendeka amesema zoezi limeanza kuleta matumaini kwa kuwa idadi kubwa ya wadaiwa wamejitokeza kulipa pamoja na kusaini mkataba wa lini watakamilisha madeni yao na kudai kwamba kiasi ambacho hakija lipwa hadi sasa ni zaidi ya bil 1.1.
Katika hatua nyingine Olesendeka amesema baada ya kusikiliza maombi ya wadaiwa ambao wamekiri kulipa fedha pindi watakapo uza dhamana zao ,amekubari kuongeza siku 23 kutoka 14 alizotoa awali kwa wadaiwa wote kurejesha fedha walizokopa katika muda huo na kudai kwamba yeyote ambaye hafika kusaini makubaliano wafike katika ofisi za wakuu wa wilaya ili kuwasilisha madeni yao.
Mara baada ya kumalizika kwa muda wa mwisho wa nyongeza mdaiwa yeyote ambaye atashindwa kulipa atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kuingizwa katika orodha ya wahujumu uchumi na kuwafungulia kesi.