Na Mwamvua Mwinyi,Mafia
KISIWA Cha Mafia kinatarajia kupata ugeni mkubwa wa watalii kupitia meli kubwa ya kitalii Afrika Kusini, itakayobeba watalii 150 ,mwezi March mwaka 2024.
Ugeni huo ni matokeo chanya ya tamasha kubwa la Utalii na Uchumi wa Bluu ambalo limefanyika hivi karibuni ,Utende wilayani Mafia .
Taarifa hiyo njema ilitolewa na Mgeni kutoka Meli ya Watalii ya THE WORLD RESIDENCES AT SEA ,Otto Van See Westhuizen aliyefika ofisi za mkuu wa wilaya ya Mafia .
Otto Van alieleza, wamefuatilia tamasha la utalii Mafia na filamu ya Royal Tour ambapo wamevutiwa kuja kujionea shughuli zinazofanywa na WanaMafia, tamaduni zao ,Utalii na Samaki aina ya Papapotwe anaepatikana kisiwani humo.
Alieleza ,moja ya maeneo wanayopatikana samaki Hawa ni kisiwani Mafia Tanzania, sehemu nyingine ni kama Mexico na Philipenes .
“Kisiwa hiki ni kizuri, tumeona Festival iliyofanyika, tutafurahi kuja mwezi wa tatu mwakani kuja kujionea mambo mengi na hasa masuala ya historia za kale ,tamaduni na utalii wa hapa”alisisitiza Otto Van.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa wilaya ya Mafia Olivanus Paul Thomas alieleza
,kwasasa wamejipanga kuendelea kutangaza utalii wa Mafia nje na ndani ya nchi ili kupata ongezeko kubwa la watalii.
“Kwa niaba ya mkuu wa wilaya,tumepokea mgeni huyu ,kutokea Afrika Kusini amekuja baada ya kuona festival ya Mafia, wameona ni vema kuja wenyewe kufanya utalii,Haya ni matokeo chanya ambayo kwetu sisi ni tija katika kutuongezea pato na kukuza utalii na uchumi wa Mafia”
“Amekuja pia kuona mandhari ya miundombinu ili waweze kuleta meli hiyo kubwa itakayobeba watalii 150 “alifafanua Olivanus.
Vilevile Olivanus anaeleza, ni wakati sasa wa kujiandaa kibiashara, uwekezaji wa usafirishaji ili kuifungua Mafia kwa ajili ya ongezeko la watalii .
Aidha alieleza kwamba, asilimia 70 ya mapato halmashauri ya Mafia inategemea utalii na uchumi wa bluu hivyo ili kufikia lengo kupitia utalii ni lazima kuongeza nguvu ya kujitangaza kiutalii kuvutia watalii.
Olivanus alisisitiza, Mafia ni kivutio cha uwekezaji katika uchumi wa bluu, ikiwemo uvuvi endelevu, ufugaji wa viumbe maji, viumbe bahari,utalii na usafirishaji baharini.