Baadhi ya majengo ya utawala ya Bandari ya Karema iliyopo wilayani Tanganyika mkoani Katavi.
Na Zillipa Joseph, Katavi
Licha ya mwaka mmoja kupita tangu bandari ya KAREMA iliyopo wilaya ya Tanganyika kuanza kazi, shughuli zake zimekuwa zikidorora kufuatia changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa meli kubwa katika ziwa Tanganyika, ubovu wa barabara ya Mpanda Karema yenye urefu wa zaidi ya kilometa mia moja na ukosefu wa reli.
Akitoa taarifa kwa Waziri wa Uchukuzi aliyefanya ziara ya ukaguzi wa bandari hiyo, Meneja wa bandari za Ziwa Tanganyika Denis Mabula alisema tangu septemba mosi mwaka jana wameweza kusafirisha mzigo wa Tani 1,500 tu.
Aliongeza kuwa bandari hiyo imekamilika kila kitu kwa aailimia mia.moja lakini changamoto hizo zinapelekea kukosa mapato.
Bandari hiyo ilijengwa kwa shilingi bilioni 47.
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame MBARAWA alisema serikali kwa kujali uwekezaji huo mkubwa itaweka lami katika barabara ya Karema, pamoja na kutengeneza meli mbili
Profesa Mbarawa alifafanua kuwa wataweka lami kipande hicho cha barabara japo si chote kwa mara moja na tayari mpango huo unafanyiwa kazi na wanachosubiri ninkutangaza zabuni tu.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tanganyika ONESMO Buswelu amewataka wasafirishaji wanaotumia ziwa Tanganyika kutumia bandari ya Karema badala ya kushusha katika bandari bubu.
Akizungunza kwa niaba ya mkurugenzi wa TASAC ambao ni wasimamizi wa usafirishaji majini, Mkurugenzi wa huduma za biashara ya meli Nelson Mlali amepongeza uwekezaji uliofanyika Karema.na kuongeza kuwa bandari hiyo ni nzuri na ikiweza kufanya kazi kwa asilimia mia moja itapunguza kero wanazopitia sasa wasafirishaji wa mizigo.
Ameongeza kuwa matazamio yao ni bandari ya Karema kuweza kuunganishwa vizuri na barabara na reli ambapo kero za usafirishaji zitapungua hususan kwa mzigo upelekwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
‘Hapa usalama upo wa kutosha na mpaka sasa hatujakutana na changamoto za ajali majini’ alisema Mlali.
Naye mbunge wa jimbo la Mpanda Magharibi Selemani Kakoso ameiomba serikali kukarabati meli zilizopo ili ziendelee kufanya kazi wakati tukisubiri kutengeneza meli mpya.