Na Mwandishi wetu, Kiteto
MBUNGE wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, Wakili msomi Edward Ole Lekaita Kisau amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha nyingi na kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo Jimboni humo.
Ole Lekaita ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mbio za mwenge wa uhuru Wilayani Kiteto wakati wa kukagua, kuzindua, kutembelea na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi ya maendeleo mbalimbali ya thamani ya shilingi bilioni 2.4.
Miradi iliyotembelewa na mwenge wa uhuru mwaka 2023 Kiteto ni pamoja na kufungua madarasa mawili na ofisi ya shule ya msingi Esukuta na daraja Orkine.
Mwenge ulifungua shule mpya ya msingi Azimio na kupanda miti 500 na kuzindua na utunzaji wa mazingira shule ya sekondari NASA Matui na kuzindua klabu ya wapinga rushwa.
Pia, mwenge wa uhuru uliweka jiwe la msingi ujenzi wa majengo matatu hospital ya wilaya ya Kiteto na kuzindua mradi wa maji wa RUWASA Majengo mapya Kata ya Kaloleni.
Ole Lekaita amesema kupitia miradi mbalimbali iliyotembelewa na mwenge Kiteto na mingine iliyopo Kiteto ambayo haijapitiwa na mwenge, wamepiga hatua kubwa ya maendeleo hivyo wanamshukuru Rais Dkt Samia.
“Kwa niaba ya watu wa Jimbo la Kiteto nampongeza Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za maendeleo zilizofanikisha miradi ya sekta ya elimu, afya, maji, miundombinu na mengine,” amesema Ole Lekaita.
Hata hivyo, amesema wakazi wa Kiteto hawana cha kumlipa Rais Samia ila wanamuombea afya njema, uzima na wanasubiri ifikapo mwaka 2025 kura zake zote za ndiyo wanazo wamezificha kwenye rubega.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2023, Abdalah Shaibu Kaim, amempongeza mbunge wa Kiteto kwa kushiriki mwanzo mwisho kwenye shughuli za mwenge ulipokuwa Kiteto.
“Mheshimiwa Mbunge Ole Lekaita nakupongeza sana kwa kushiriki ipasavyo kwenye mbio za mwenge kwa mwaka huu wewe ni mzalendo mtu bingwa kabisa kwani umeonyesha ushirikiano mkubwa na viongozi wenzake wa Kiteto,” amesema Kaim.