Na Mwamvua Mwinyi, Mkuranga
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge ,amewaasa wakulima wa zao la Korosho ,kuhakikisha wanalima kilimo cha kisasa chenye tija ili kupata korosho zenye ubora na kujiongezea kipato.
Aidha ametoa rai kwa wataalamu wa kilimo kuwa na mkakati utakaoweza kuwasaidia wakulima kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo.
Kunenge alitoa rai hiyo Oktoba 5, wakati akifungua mkutano wa wadau wa korosho mkoa wa Pwani ,uliofanyika katika Ukumbi wa Flex Garden Wilayani Mkuranga.
Aliwataka wakulima hao kuhakikisha wanajifunza kupitia kwa wenzao wa sehemu nyingine ili kuhakikisha wanaleta tija katika zao hilo.
“Kujifunza sio kosa , hivi kunashida gani tukapata mkulima mmoja anaefanya vizuri aje hapa tukajifunza kupitia yeye ili tuweze kufikia malengo na kufanya kilimo chenye tija.”
“Ni matarajio yangu ifike mahala nikiambiwa eneo fulani wanazalisha korosho ,tija tunaona bado mkorosho mmoja unazalisha wastani wa kg 20,Tunadhani waingie wataalamu waangalie changamoto ni nini kama aidha aina ya miche aliyopanda ama afya ya udongo au ni madawa”
“Bila kufanya hivyo tutakuwa tunapiga kelele bure wakati mkoa wetu tunauendesha kitaalamu” alisema Kunenge.
Akizungumzia mfumo wa stakabadhi ghalani anaelekeza kuwa kama mfumo huo unatija ,iangaliwe namna ya mazao mengine ya biashara yaingie katika mfumo huo.
“Dunia ya leo hakuna mwananchi atakaekataa kitu kinachompa tija na maslahi ,wakulima hawa wanataka kubadili maisha yao kama kitu ni kizuri na kina maslahi mazuri kwake hawezi kukataa ” alieleza Kunenge.
Vilevile aliwataka watendaji kuhakikisha wanasajili wakulima wote ili kuhakikisha wanapata pembejeo.
Pia Kunenge aliviasa Vyama vya Ushirika vinavyosimamia mazao hayo kuhakikisha wanasimamia bei nzuri ya mazao hayo ili kuhakikisha wakulima wanapata faida.
Akiwasilisha taarifa ya ukusanyaji na uuzaji wa Korosho na Ufuta kwa mwaka 2022/2023 ,Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika (CORECU ) ,Mantawela Hamis alisema ,Chama kwa kushirikiana na Sekretariet ya Mkoa kiliendesha jumla ya minada 9 ya Korosha ambapo vyama vya msingi 75 vilihusika katika kukusanya na uuzaji wa Korosho.
Anasema Jumla ya tan 12,151.339 ambapo tani 10,759.449 ziliuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na tani 1,391.840 ziliuzwa kwa wabanguaji wa ndani kupitia soko la awali chini ya usimamizi wa Halmashauri.
Alieleza ,Bei ya juu ya wastan kwa korosho za daraja la kwanza ilikuwa ni sh. 1,892.92 na bei ya chini ya wastani daraja hilo ilikuwa ni sh.1,421.00 na daraja la pili ziliuzwa kwa bei ya juu wastani ya sh.1,520.00 na bei ya wastani ilikuwa sh. 1,202.02.
Mantawela alieleza ,thamani ya mauzo yote kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ni sh.Biln 18,789,041,912.
Anasema ,ubora wa korosho umeongezeka kutoka asilimia 72 msimu 2021/2022 na kufikia asikimia 96.3 msimu 2022/2023 .
Mantawela alibainisha kwamba, kati ya kilo 10,759,499 zilikusanywa ghalani na kilo 10,361,124 sawa na asilimia 96.3 ni daraja la kwanza na kilo 398,375 sawa na asilimia 3.7 ni daraja la pili.