Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary M. Mwanjelwa (Mb) akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Mhe. Omary Ahmed Badwel Bungeni leo jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililohusu Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika vijiji vyote nchini.
*********************************
Na. Aaron Mrikaria-Dodoma
Serikali imewaagiza Viongozi wa Vijiji kutowalazimisha walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kukatwa ruzuku kwa ajili ya kuchangia bima za afya na michango mbalimbali ya kijamii kwani ruzuku hiyo hutolewa na Serikali kwa ajili ya kuziwezesha kaya maskini kujikwamua kiuchumi.
Agizo hilo limetolewa Bungeni leo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kwa
niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Kapt.
(Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Bahi,
Mhe. Omary Ahmed Badwel aliyetaka kujua Utekelezaji wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini katika vijiji vyote nchini.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, ruzuku inayotolewa na Serikali kwa walengwa
ni kwa ajili ya kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi kama vile chakula,
gharama za elimu na Afya na kuwekeza katika kuanzisha miradi
itakayowaongezea kipato na hatimaye kujikwamua na umaskini, hivyo ni
maamuzi ya kaya husika kupanga matumizi ya ruzuku wanayoipata.
“Katika baadhi ya maeneo, Viongozi wa Vijiji wamekuwa wakiwalazimisha
walengwa kukatwa ruzuku ili kulipia bima za afya na michango mbalimbali jambo ambalo si sahihi na halikubaliki”, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amefafanua.
Aidha, Dkt. Mwanjelwa ameelekeza walengwa kutokatwa ruzuku moja kwa moja
bila ridhaa yao bali wapewe stahiki zao na kama kuna michango ya shughuli za
maendeleo ya kijiji inapaswa kutozwa kwa wananchi wote wa kijiji husika.
Dkt. Mwanjelwa amewataka viongozi wote waliokuwa wanatoa amri ya kukatwa
kwa ruzuku za walengwa wa TASAF moja kwa moja bila ridhaa yao, waache
mara moja kwani ni kinyume cha utaratibu na iwapo wataendelea, Serikali
itawachukulia hatua za kali za kinidhamu na kisheria.
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini tangu uanze kutekelezwa na Serikali mwaka
2013 umezinufaisha kaya maskini kwa asilimia 70, na hivi sasa Serikali
inajiandaa kuanza utekelezaji wa Awamu ya Tatu sehemu ya pili mwishoni mwa
mwaka huu baada ya Serikali kupata fedha lengo likiwa ni kuzifikia kaya zote
maskini nchini