Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akiwasili katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizopo katika mpaka wa Tanzania na Malawi wa Kasumulu Wilayani Kyela, mkoani Mbeya. Kushoto kwake ni Meneja Msaidizi wa Fordha kutoka Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mbeya, Bw. Nsajigwa Mwambegele.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akisani kitabu cha wageni katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizopo katika mpaka wa Tanzania na Malawi wa Kasumulu Wilayani Kyela, mkoani Mbeya.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akiongea na wananchi wa Kitongoji cha Kilambo, Kata ya Njisi, Wilani Kyela (Hawapo pichani) mara baada ya kutembelea na kukagua shughuli za kiuchumi na maendeleo katika mpaka wa Tanzania na Malawi wa Kasumulu, mkoani Mbeya. Kulia kwake ni Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) na kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kyela,Bw. Elias Mwanjala.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, akifuatilia Mkutano wa Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu ((Mb), uliofanyika Wilayani Kyela mkoani Mbeya. Kulia kwa Bw. Mwandumbya ni Naibu Kamishina Mkuu kutoka Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Mcha Hassan Mcha na anayefuatia ni Mbunge wa Jimbo la Kyela, Mhe. Ally Mlagila Jumbe.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) akifurahia jambo wakati wa Mkutano na wananchi wa Kitongoji cha Kilambo, Kata ya Njisi Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya. Kushoto kwa Mhe. Dkt. Nchemba ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kyela Bw. Elias Mwanjala na kulia ni Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) na anayefuatia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF, Kyela)
Na Ramadhani Kissimba, WF, Kyela
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameiagiza Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA), kusaidia kukuza Sekta Binafsi nchini ambayo itasaidia kuongeza kipato, kukuza uchumi wa nchi na itatoa fursa kwa vijana wengi kujiajiri.
Mhe. Dkt. Nchemba alitoa maagizo hayo wakati akiongea na wananchi wa Kilambo, Kata ya Njisi Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya, mara baada ya kufanya ziara yake ya kukagua shughuli za kiuchumi na maendeleo katika Kituo cha Forodha cha Pamoja-Kasumulu kilichopo mpakani mwa Tanzania na Malawi.
Alisema kuwa dhamira ya nchi ni kutaka kukuza Sekta Binafsi, hivyo ni lazima kuwe na nidhamu katika kuisimamia Sekta Binafsi hasa kwa kulinda mitaji ya vijana walioamua kujiajiri na kuajiri vijana wenzao na si kuua mitaji yao.
‘’Ni lazima tuwe na nidhamu katika sekta binafsi na tuache ubosi katika mitaji ya watu, na kama kijana ameamua kuanzisha shughuli yake na hajaisajili msimfungie biashara badala yake mleteeni hiyo leseni ambayo hana, msiharibu mtaji wake ili vijana wengi wajiajiri’’ alisema Mhe. Dkt. Nchemba
Aidha, Mhe.Dkt. Nchemba aliwataka wananchi kujenga tabia ya kulipa kodi na kuheshimu sheria za nchi ili kuongeza idadi ya walipa kodi, jambo ambalo litasaidia kushusha viwango vya ulipaji kodi na kuwapunguzia mzigo mkubwa wale wanaolipa kodi.
Aliongeza kuwa matamanio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuona viwango vya kodi vinashuka ili kuchochea maendeleo ya kila Mtanzania.
‘’Natoa rai hapa wakati tunawasisitizia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutekeleza maelekezo ya Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kukusanya mapato kwa weledi na kufuata kanuni, tunawasisitiza pia wananchi mjenge utaratibu wa kulipa kodi, kuheshimu sheria ili tunapokwenda! tukilipa wengi, tuweze kushusha viwango vya kodi’’ Aliongeza Mhe. Dkt. Nchemba
Awali akizungumza na Uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya, Mhe. Dkt. Nchemba aliwataka kuhakikisha wanadhibiti na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaofanya biashara za magendo katika mpaka wa Kasumulu, vitendo vinavyoikosesha Serikali mapato.
Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Nchemba aliongozana na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb), Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoani humo.