


Baadhi ya waumini wa Dini ya Mashahidi wa Yehova mkoani Mbeya, Watafsiri wa lugha ya alama na viziwi wakiendelea kupeana elimu ya Biblia katika kambi iliyopigwe kwenye viwanja vya Ruandanzovwe ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa waumini hao kwenye Wiki ya kuelekea siku ya Viziwi Duniani ambapo kitaifa itafanyika mkoani humo. (Picha na Joachim Nyambo)
Na Joachim Nyambo, Mbeya.
JAMII imeaswa kutowaficha majumbani viziwi na badala yake kuwawezesha kunufaika na fursa zinazowazunguka kwenye maeneo yao ili kutowafanya wanyonge na wenye kujiona wanatengwa.
Miongoni mwa fursa wanazopaswa kunufaika nazo ni pamoja na za mafundisho ya kidini yenye kuwawezesha kuishi kwa kumtumikia mwenyezi Mungu na kuishi maisha yenye amani na upendo kwa kushirikiana kwa karibu na wanajamii wengine.
Waumini wa Dini ya Mashahidi wa Yehova mkoani Mbeya walibainisha hayo kwenye Kambi maalumu ya utoaji Mafundisho ya Biblia kwa Viziwi inayoendelea katika Viwanja vya Ruandanzovwe jijini hapa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Viziwi Duniani itakayofanyika kitaifa mkoani Mbeya kesho.
Msemaji wa Dini ya Mashahidi wa Yehova Mkoa wa Mbeya, Jovenary Joseph alisema katika kushiriki wiki ya Viziwi duniani wanatarajia kufikisha mafundisho ya Biblia kwa zaidi ya viziwi 500 wanaotarajiwa kuja mkoani hapa kwaajili ya kushiriki maadhimisho ya kilele cha siku ya viziwi Kitaifa.
Joseph alisema kwa kutambua Mungu wanayemtumikia Mashahidi wa Yehova hana ubaguzi kwakuwa anawajali watu wake wa namna zote wameamua kujikita kwenye utoaji elimu ya Biblia kwa njia ya ishara kwa viziwi wakitambua kuwa kundi hilo pia linalo uhitaji mkubwa wa kuyajua mafundisho yake.
“Tunatoa elimu ya Biblia kwa njia ya ishara ili kuwafikia viziwi waliopo hapa mkoani Mbeya na wale watakaokusanyika kutoka maeneo mbalimbali kuja kwenye maadhimisho ya siku ya viziwi duniani kitaifa hapa.” Alisema Joseph
“Viziwa pia wanao uhitaji wa kufikiwa na habari za ufalme wa Mungu au neon lake kwa ujumla. Wakijifunza neon la Mungu kupitia lugha yao inaweza kuwa rahisi kuifikia mioyo yao na wanaweza kuhisi kuwa pamoja na Mungu.”
Msemaji huyo alisema tafiti zinaonesha watu walio na mahitaji ya kipekee wakiwemo viziwi na makundi mengine ya namna hiyo ndani ya jamii waishi kwa kuhisi wanatengwa na kutothaminiwa hivyo ni muhimu kufikiwa na kushirikishwa kwenye mambo muhimu ikiwemo kulifahamu neno la Mungu.
Muumini mwingine wa Dini hiyo, Elisha Mwakapombe ambaye pia ni mtafsiri wa lugha ya ishara kati ya wafundishaji na viziwi alisema wanatoa huduma ya mafundisho ya Elimu ya Biblia kwa kundi hilo bila malipo ili kuliwezesha kuwa na ustawi wa kiroho sawa na wana jamii wengine.
Mwakapombe alisema kupitia mafundisho hao wanawafundisha viziwi kuwa mama bora, baba bora na pia watoto bora hivyo kuweza kuwa na familia inayojitambua sambamba na yenye kuthamini umuhimu wa kujitegemea kwa kufanya kazi na kuepuka utegemezi.
Mtafsiri mwingine, Pili Costantine alisema ni wakati kwa wazazi na walezi walio na viziwi majumbani kuwaruhusu watoto au vijana wao kushirikiana na wenzao kwenye ujifunzaji wa mambo mbalimbali yakiwemo yanayomhusu Mungu.
Wanufaika wa mafundisho hayo yanayotolewa kwa njia ya ishara Happy Antony mkazi wa Shewa na Gwamaka Alfonce wa Ilemi wote jijini Mbeya walisema wanajihisi kupata faraja kubwa mionyoni mwao tangu walipojiunga na huduma ya mafunzo ya biblia.
Wanufaika hao walisema awali walishindwa kujifunza elimu ya biblia kwakuwa jamii iliyowazunguka haikuwa na uwezo wa kuwasiliana nao na hata ndugu na jamii walioweza kuzungumza nao baadhi hawakuwa na ufahamu juu ya neon la Mungu wala mafundisho ya Biblia.