**************************************
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela chilumba, ameagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa na wavuvi wote kuwapo na Soko la kuuza Samaki kwa kipindi cha siku saba.
Ameyasema hayo hivi karibuni wakati akiongea, katika mkutano wa Hadhara wenye lengo la kutatua changamoto za kutokuwepo kwa soko la samaki,na ulinzi na usalama wa wavuvi, uliojumuisha wavuvi, na wafanyabiashara ya Samaki, uliofanyika eneo la” fisheries” Mbamba- bay Wilayani hapa.
Bi Chilumba alifafanua kuwa, kwa muda mrefu Wilaya ya nyasa haina soko la samaki, hata mgeni akija hajui wapi ni sehemu ya kununua samaki. Anabaki kusubiri yeyote atakayepita kwa bahati ili anunue.Imefika wakati wavuvi ,wachuuzi wa samaki na dagaa tukubaliane wapi iwe ni sehemu maalumu ya kuuzia samaki, ili atakayekaidi uamuzi huu achukuliwe hatua.
Aliongeza kuwa amelazimika kuwafuata na kufanya mkutano wa wadau wa mazao ya uvuvi ili Kutatua changamoto, ya kutokuwa na sehemu maalumu ya kuuzia samaki katika maeneo ya Wilaya ya Nyasa.
“Nimelazimika kuwaita leo, kwa ajili ya kuongea nanyi kwa lengo la kutatua tatizo la kutokuwa na sehemu maalumu ya kuuzia samaki, katika Wilaya yetu ya Nyasa inayofunguka kwa miundombinu ya barabara, umeme na Bandari.
Tunalazimika kuwa na sehemu hii ya kuuzia samaki, kwa sababu hata wageni kwa sasa wakija hajawajui wapi kwa kupata samaki, wanabaki wanasubiri kwa wachuuzi ambao wanatokea kwa bahati .Leo tukubaliane na tuwe na
sehemu maalumu ya kuuzia samaki ili tuweze kuwa na maendeleo katika Wilaya yetu.
Wavuvi wa Mbamba-bay, wataja changamoto iliyowafanya wasiwe na soko la samaki, ni hawakupata elimu ya kuwa na soko la Samaki hali iliyowasababisha kila mtu kuvua na kuuza peke yake.Lakini mara baada ya Elimu hiyo wako tayari kuwa na soko la Samaki na hakuna mtu atakayeuza sehemu nyingine.
Mkutano huo umeazimia kuwa eneo la “fisheries” Mbamba-bay liwe eneo la Soko la samaki na Lianze kutumika mara moja. Changamoto zingine zitatuliwa wakati wauzaji wote wa samaki wakiwa katika eneo hilo maalumu la kuuzia samaki.
Aidha wavuvi hao wamempongeza Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela chilumba kwa kuwa karibu na wavuvi hao na kuwatembelea mara kwa mara na kuhakikisha anawatatulia changamoto mbalimbali zinazo wakabili katika maeneo yao ya kazi.
“Sisi wavuvi tunakupongeza sana mkuu wa wilaya yetu kwa kututatulia changamoto mbalimbali.umetupa injini za boti( 13) kwa ajili ya uvuvi, na umekuwa karibu nasi kwa masuala ya ulinzi na usalama wetu kipindi tunapokuwa na matatizo au kututembelea , kubaini na kutatua changamoto mbalimbali zinazotukabili. Sisi tunakupongeza sana na tunaomba
utufikishie salamu zetu Kwa Mh. Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John pombe Magufuli kwa kutujali sisi wavuvi. Shukrani zetu atazipata kwa kumpa kura zetu , tukianza na uchaguzi wa Serikali za mitaa kamwe hatutamwangusha” . Alisema mwenyekiti wa wavuvi Pita
sumuni.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nyasa Benward Semwaiko ambaye pia ni Mkuu wa idara ya mifugo na uvuvi Wilaya ya Nyasa, wakati akimshukuru Mkuu wa wilaya ya Nyasa, amesema atahakikisaha ndani ya siku saba soko la samaki litakuwa limeanza na kutatua kero ya kuadimika kwa samaki, kwa kuwa muda wote samaki watakuwa wanapatikana katika soko la Samaki la Mbambabay Wilayani Nyasa.
Aidha amewataka wavuvi kutii agizo hilo kwa kuwa ni makubaliano ya pande zote mbili kati ya Serikali Wilayani hapa na Wavuvi wote wa Wilaya ya Nyasa,kwa kuwa lengo ni kuboresha kipato kwa wavuvi hao na kuwatengenezea Soko la Uhakika kwa siku zote.