Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mkuu wa mkoa wa Pwani,Abubakari Kunenge ametoa rai , kwa Uongozi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF )kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu ili kuepusha upotevu wa fedha za Serikali.
Alitoa rai hiyo,wakati akifungua mafunzo kwa wakuu wa Usalama Barabarani wa Jeshi la Polisi Tanzania kutoka Wilaya za kipolisi Mkoa wa Pwani na Dar es salaam katika ukumbi wa Wauguzi uliopo Mjini Kibaha.
Vilevile Kunenge, aliutaka Mfuko huo kuendelea kutenda haki kwa kufuata sheria kanuni na taratibu bila kufanya upendeleo au kumpunja mtu yeyote pale anapodai haki au fidia yake.
Alitoa rai kwa maafisa hao wa usalama barabarani kutoa ushirikiano kwa mfuko huo wa WCF pindi wanapohitaji taarifa sahihi za muathirika wa ajali ili taratibu zikamilike.
Katika hatua nyingine, Kunenge aliupongeza mfuko huo kwa kuweza kutoa mafunzo hayo kwa maafisa hao ambayo ni muhimu kwa pande zote ikiwa ni moja ya njia ya maboresho na uimarishaji utendaji kazi wa taasisi za Serikali.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya WCF, Emmanuel Humba alisema kuwa, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa kazi kati ya Jeshi la Polisi na Mfuko huo.
Aliongeza kuwa WCF inafanya kazi kwa karibu na Jeshi la Polisi, hivyo amelitaka Jeshi hilo kikosi cha usalama barabarani kutoa taarifa sahihi za mtu anaepata ajali.
Mafunzo ya aina hii yalishatolewa kwa wakuu wa Jeshi la Polisi kwa Makamanda wa Mikoa na sasa ni kwa Wakuu wa Usalama Wilaya wakianza na wa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.