Wakaguzi wa Ndani katika Taasisi za Umma wametakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, wakati wa ukaguzi wa miradi na mifumo mbalimbali ya TEHAMA kwenye taasisi zao, ili kuhakikisha wanatenda haki.
Wito huo umetolewa na wakati wa ufunguzi wa awamu ya nne ya mafunzo maalum kuhusu ukaguzi wa mifumo na miradi ya TEHAMA kwa wakaguzi wa ndani kutoka katika Taasisi za Umma 102 yanayofanyika jijini Arusha.
βIli muweze kufanya kazi zenu za ukaguzi wa mifumo kwa weledi na kutoa ushauri wenye tija kwa serikali, ni lazima kila mkaguzi afahamu kwa kina Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, ambayo itawaongoza katika kurahisisha kazi yenu na kuweza kufanya ukaguzi wa mifumo na miradi ya TEHAMA kwa weledi na kuzingatia hakiβ, alisema Mwamnyasi.
Aliongeza kuwa, kada ya ukaguzi ni moja ya kada muhimu katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Serikali hivyo, utaratibu wa kupatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo na ujuzi zaidi Wakaguzi wa Ndani utakuwa ni endelevu hususan kwenye eneo la TEHAMA kwakuwa utendaji kazi wa Serikali wa sasa ni wa kidijitali.
Meneja wa Kitengo cha Huduma za Sheria cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ACP. Raphael Rutahiwa, aliwahimiza wakaguzi hao kuhakikisha wanatumia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao wakati wa kusimamia na kufanya ukaguzi wa miradi na mifumo mbalimbali ya TEHAMA katika taasisi zao.
βKama Mkaguzi wa Ndani ukiijua Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa undani itakusaidia kuweza kufanya ukaguzi wa mifumo na miradi ya TEHAMA kikamilifu, kwa uhuru na kutoa ripoti zenye haki bila kufungamana na upande wowoteβ, alisema Rutahiwa.
Pia, aliwakumbusha Wakaguzi hao kuhakikisha kuwa kila mradi au andiko la mradi wa TEHAMA lililoanzishwa linazingatia taratibu za utendaji kazi wa taasisi husika na kabla ya utekelezaji wake liwasilishwe e-GA ili liweze kupata kibali cha kuendelea na utekelezaji.
Naye Meneja wa Udhibiti wa Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao Bi. Sultana Seiff, alisema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha wakaguzi wa ndani kufanya ukaguzi katika eneo la TEHAMA kwa ufanisi mkubwa na kuhakikisha Taasisi za Umma zinazingatia Sheria ya Serikali Mtandao, Kanuni zake, Viwango na Miongozo iliyopo ili kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma kama ilivyokusudiwa.
Jumla ya Wakaguzi wa Ndani kutoka katika Taasisi za Umma 102 zikiwemo Mamlaka za Maji, Vyuo Vikuu na Taasisi nyingine za Umma wanashiriki mafunzo hayo ya siku nne yanayotarajiwa kukamilika Septemba 28, mwaka huu.
Mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo yanatolewa na e-GA kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, ambapo hadi sasa zaidi ya Wakaguzi wa Ndani 355 kutoka katika taasisi mbalimbali za umma wamepatiwa mafunzo hayo.