Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Mwanafunzi kidato cha pili , Shule ya Sekondari Nyumbu, Kibaha Mkoani Pwani Warda Machamula (16) amepotea kusikojulikana miezi mitano sasa ,tangu april 21, 2023.
Uchunguzi wa awali umebaini binti huyo ametoweka nyumbani baada ya kuadhibiwa kwa kuchapwa na mama mlezi wake aliyekuwa anakaa nae kwa takriban miaka sita.
Kamanda wa polisi Mkoani Pwani,Pius Lutumo akithibitisha juu ya tukio hilo, alieleza binti huyo aliadhibiwa na mlezi wake kwa kosa la kumiliki simu ya mkononi kwa kificho.
“Tarehe 21.4.2023 tulipokea taarifa ya kutoweka kwa mwanafunzi Warda Machamula ikiwa ni taarifa ya kawaida ya kupotea kwa mtu jambo ambalo ni kawaida kwa familia nyingi kutoa taarifa pale wanapopotelewa na mtu kwenye familia zao”
“Tarehe 18.5.2023 baba mzazi wa mtoto Warda alifika kituo cha polisi wilaya ya Kibaha kutoa taarifa upya ya upotevu wa binti yake hali iliyopelekea jeshi la polisi kufungua jalada la uchunguzi”
Lutumo alieleza, jeshi la polisi lilifungua jalada hilo lengo kubaini sababu za kupotea,kubaini sababu za mtoto kutokaa na wazazi wake miaka sita.
Pia kubaini mahali alipo binti huyo na namna ya kumpata.
Lutumo alifafanua, jeshi la polisi lilimkamata mtuhumiwa ambae ni mama mlezi wa Warda akahojiwa na baadae kuachiwa kwa dhamana kwa mujibu wa sheria za makosa ya jinai.
Mtuhumiwa ambae ni mwalimu amekuwa akiishi na mtoto huyo tangu mwaka 2018 akiwa darasa la nne huko Bungu, Mkuranga baada ya mama mzazi wa Warda kumkabidhi mtoto ili aweze kufanya mtihani wa darasa la nne iliyokuwa mbele yake baada ya mtihani huo Warda aliendelea kuishi na mlezi wake hadi 21.4.mwaka huu alipotoweka.
Jeshi la polisi kwa kushirikiana na wadau wa mifumo ya kiuchunguzi linafanya uchunguzi kwa kasi ili kubaini alipo binti huyo na kumweka kwenye mikono salama.