Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama akisikiliza maelezo kuhusu mradi wa lambo katika Kijiji cha Melela Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro alipofanya ziara ya kukagua Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR).
Muonekano wa lambo la kuvunia maji ambalo ni mkombozi kwa wakazi wa Kijiji cha Melela Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro alipofanya ziara ya kukagua Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR).
Sehemu ya mbogamboga zinazolimwa katika kitalu nyumba katika Kijiji cha Ng’hambi Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) ambao umejenga kisima kirefu kinachosaidi katika umwagiliaji wa mbogamboga hizo.
…………..
Wakazi wa vijiji vya Kazania Wilaya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma na Melela Wilaya ya Mvomero, Morogoro wametakiwa kutunza na kuendeleza Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) ili kukabiliana na ukame.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama alipofanya ziara na kukagua miradi ya kilimo cha mbogamboga kupitia kitalu nyumba, ufugaji wa nyuki na ujenzi wa kisima katika vijiji hivyo inayotekelezwa na EBARR kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais.
Amewataka wakazi hao kuwa wamoja kwa kuepuka majungu na fitina hasa katika kipindi cha sasa walichoanza kupata kipato kutokana na uzalishaji wanaoufanya.
Dkt. Mkama amesema kwenye miradi ya kujipatia fedha kwa wananchi wenye ushirikiano kumekuwepo na sintofahamu hali inayosababisha fitina na majungu hivyo kukosekana kwa amani.
“Ndugu zangu nawaomba msiruhusu kabisa kutokea kwa hali hii na endapo kutatokea malalamiko kuhusu matumizi mabaya ya fedha mntakiwa kufanya uchunguzi na sio kukurupuka kutoa maamuzi kwa kuwa kwenye wengi kuna mengi,“ amesema.
Pia, Dkt. Mkama amewahimiza wananchi kutumia miundombinu inayojengwa ikiwemo visima virefu hatua itakayonusuru mito miwili katika Wilaya ya Mvomero.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wilayani Mvomero akiwemo Fatuma Hamisi wamesema Mradi wa EBARR umekuwa manufaa kwao kwani umewaondolea changamoto mbalimbali.
Wamesema awali walikuwa wanalima mbali na makazi yao ambapo mashamba yao yalikuwa yakivamiwa na tembo, hivyo tangu mradi uanze kutekelezwa wanalima karibu kwa kufanya kilimo cha umwagiliaji.
“Zamani kilimo cha mbogamboga kilikuwa ni kigumu kwani tulikuwa tunategemea maji kutoka kwenye vyanzo vya mito ambayo kwa sasa imekauka lakini baada ya kupata Mradi wa EBARR tumechimbiwa kisima na sasa tunapata maji ya kutosha na kilimo kinaendelea,“ amesema mkazi wa Kata ya Lubungo Wilaya ya Mvomero Bw. Malegesi Chilongo
Hala kadhalika, wameishukuru Serikali kwa kutoa ekari 10 kwa ajili ya wananchi kulima mbogamboga hivyo kuweza kujipatia kipato ambacho kinawasaidia kujikimu.
Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto ya kidunia inayokabili pia baadhi ya maeneo nchini na kusababisha ukame na mafuriko hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inaratibu Mradi wa EBARR ukifadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) chini ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).
Mbali ya wilaya za Mvomero na Mpwapwa pia mradi huu pia unatekelezwa katika wilaya za Simanjiro (Manyara), Kishapu (Shinyanga) na Kaskazini ‘A‘ Mkoa wa Kaskazini – Unguja.
Kupitia mradi huo wananchi wa nmaeneo yenye ukame wanawezeshwa kujipatia kipato kwa njia mbadala bila kujihusisha na vitendo vya uharibifu wa mazingira vikiwemo ukataji miti kwa ajili ya nishati na unyweshaji wa mifugo kwenye vyanzo vya kwa kuwa wanajengewa miundombinu kwa ajili hiyo.