Rais Dkt. John Magufuli akimuapisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) Charles Kichere wakati wa hafla ya kuwapisha Viongozi na
Watendaji mbalimbali wa Serikali aliowateua mwishoni wa wiki. Hafla hiyo
iilifanyika leo Jumatatu (Novemba 4, 2019) Ikulu Jijini Dar es Salaaam.
Rais Dkt. John Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Makamu Mwenyekiti wa
Tume ya Haki za Binadamu naUtawala Bora (THBUB) Mohamed Khamis
Hamad mara baada ya kumuapisha katika hafla ya kuwaapisha Viongozi na
Watendaji mbalimbali iliyofanyika leo Jumatatu (Novemba 4, 2019).
Rais Dkt. John Magufuli akisalimiana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan mara baada ya kuwaapisha Viongozi na Watendaji mbalimbali katika
hafla iliyofanyika leo Jumatatu Novemba (4, 2019) Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
Rais Dkt. John Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mara
baada ya kuwaapisha Viongozi na Watendaji mbalimbali katika hafla
iliyofanyika leo Jumatatu Novemba (4, 2019) Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Magufuli akisalimiana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof.
Ibrahim Juma mara baada ya kuwaapisha Viongozi na Watendaji mbalimbali
katika hafla iliyofanyika leo Jumatatu Novemba (4, 2019) Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
Rais Dkt. John Magufuli akiteta jambo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
mara baada ya kuwaapisha Viongozi na Watendaji mbalimbali aliwaoteua
mwishoni mwa wiki. Hafla hiyo ilifanyika leo Jumatatu Novemba (4, 2019)
Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi akisalimiana na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Serikali (CAG) Charles Kichere muda mfupi kabla ya kuapishwa na
Rais Dkt. John Magufuli wakati wa hafla ya kuwaapisha Viongozi na
Watendaji mbalimbali. Hafla hiyo ilifanyika leo Jumatatu (Novemba 4, 2019)
Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Magufuli akiwaapisha Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania wakati wa hafla ya kuwapisha iliyofanyika leo Jumatatu Novemba
4, 2019.
(PICHA NA MAELEZO)
*****************************
Na Mwandishi Wetu,
MAELEZO
DAR ES SALAAM
4.11.2019
RAIS Dkt. John Magufuli amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu mpya wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na kutambua nafasi, wajibu na majukumu yake ili kuepuka mgongano na mihimili ya Dola.
Akizungumza katika hafla ya kuwaapisha Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Serikali aliowateua mwishoni mwa wiki, Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Jumatatu (Novemba 4, 2019), Rais Magufuli alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anapaswa kutambua wajibu wake na kutekeleza maagizo na ushauri anapopewa na Viongozi wengine wa Mihimili ya Dola na sio kubishana nayo.
Rais Magufuli alisema Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ipo kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Nchi, hivyo mwenye mamlaka ya uteuzi (Rais) ana uwezo kumuondoa madarakani mteule wake kulingana na madaraka aliyonayo kupitia Katiba iliyopo hivyo jukumu alilonalo CAG ni kufanya kazi zake pasipo na kuonea watu.
‘’Unapopewa kazi usibishane na Mhimili mwingine, tambua wewe ni mtumishi wa umma kasimamie ofisi yako, una nafasi kama CAG kwa mujibu wa sheria na Katiba, lakini ni vyema ukatambua kuwa mwenye Serikali yupo pia kuna mihimili mingine ya Dola usibishane nayo’’ alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alimtaka CAG mpya Charles Kichere kuiangalia upya Ofisi hiyo kwa kuwa yapo mambo mengi mabaya yaliyokuwa yakifanywa na mtangulizi aliyepita hivyo ni vyema akashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili kufanyia kazi udhaifu mbalimbali uliokuwa ukijitokeza ambao ulikuwa ukileta taswira isiyo nzuri Ofisi hiyo.
Akitolea mfano Rais Magufuli alisema baadhi ya watendaji wa Ofisi ya CAG wamekuwa wakilipwa pesa na Ofisi hiyo kwa ajili ya kwenda kufanya ukaguzi wa fedha katika Balozi za Tanzania nje ya Nchi, lakini maofisa hao wanapofika katika Balozi hizo wamekuwa wakiomba kulipwa fedha kwa mara ya pili.
Akizungumzia Majaji wapya 12 wa Mahakama Kuu aliowateua, Rais Magufuli aliwataka Majaji hao kwenda kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili Mahakama ikiwemo utoaji wa haki kwa wakati ili kuweza kuwasaidia wananchi maskini, kwa kuwa mamlaka waliyonayo ni makubwa katika kusimamia nafasi ya utoaji haki duniani.
Aliongeza kuwa iwapo Mahakama itafanya kazi zake kwa usahihi itaweza kusaidia vizuri Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kufanya kazi zake kwa urahisi na hivyo kuwafanya wananchi kuweza kujenga imani na mhimili huo wa Dola.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma alisema nyongeza ya majaji wapya 12 wa Mahakama Kuu walioteuliwa na Rais watasaidia kuongeza kasi ya ufanisi wa utendaji kazi wa Mahakama ambapo kwa sasa idadi ya Majaji hao itafikia 78, ukiondoa majaji 2 waliopo katika kazi maalum.
Prof. Juma aliwataka majaji hao kufanya kazi kwa weledi na maarifa na kuzingatia miongozo na viapo vya maadili na uadilifu wa kazi zao, kwani wananchi wana imani kubwa na mahakama katika suala zima la utoaji wa haki kwa wananchi hususani wananchi maskini.
‘’Mnaanza kazi na mtambue kuwa mnaaminiwa na vyombo vya dola na wananchi, upo utaratibu wetu tuliojiwekea na kuusimamia, tumejipangia kusikiliza mashauri 220 kwa mwaka pamoja na kutoa hukumu kwa wakati, yote haya mnapaswa kwenda kuyasimamia’’ alisema Prof. Juma.
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai alisema Watanzania wana imani kubwa na mhimili wa mahakama katika kusikiliza na kumaliza changamoto mbalimbali ikiwemo kufanya uamuzi wa kesi mbalimbali ambazo baadhi yake zinapochelewa kukamilishwa kwa wakati zimekuwa zikisababisha idadi kubwa ya wafungwa katika magereza mbalimbali nchini.
‘’Hivi karibuni, Mhe Rais alitembelea Gereza la Butimba na alijionea idadi kubwa ya wafungwa, wapo wengine wapo kwa makosa yasiyo ya kwao na wale wasiohusika basi mahakama iharakishe kesi zao ili nao waweze kuungana upya na familia zao’’ Alisema Spika Ndugai.
Katika Hafla hiyo, Rais Magufuli aliwaapisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Majaji 12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) pamoja na Makamishina wa Tume hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Kamishina wa Kazi pamoja na Balozi wa Tanzania Nchini Kuwait.