Mnamo 22/09/2023 majira ya saa 11:40 jioni huko eneo mteremko wa Iwambi Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya katika barabara ya Mbeya kuelekea Tunduma, Gari yenye namba za usajili BCE 9384/ABX 8675 aina ya Howo mali ya kampuni ya Horn Afric Motors ltd ya nchini Zambia ikitokea Mbeya kuelekea Tunduma likiendeshwa na dereva MOHAMED ABILAH [47] Msomali, Mkazi wa Zambia iliigonga kwa nyuma Gariyenye namba za usajili T.636 DQY aina ya Mitsubish Rosa ikitokea Mbeya mjini kuelekea mbalizi ikiendeshwa na Dereva ELLY ELIA MWAKALINDILE [41] Mkazi wa Iyunga na kusababisha vifo kwa watu 9 kati yao wanaume 5 wanawake 4.
Aidha katika ajali hiyo watu 23 wamajeruhiwa kati yao wanaume 13 na wanawake 10. Majeruhi wanaendelea kutibiwa Hospitali Teule ya Ifisi iliyopo Mji Mdogo wa Mbalizi na wengine wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya. Miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali Teule ya Ifisi Mbalizi ambapo miili ya marehemu 07 imetambuliwa huku miili ya watu 02 bado haijatambuliwa.
Chanzo cha ajali hii ni Dereva wa lori kushindwa kulimudu gari lake kwenye mteremko mkali na kwenda kuigonga kwa nyuma Gari ya abiria. Dereva wa lori amekamatwa na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa madereva ambao wanapita katika Mkoa wa Mbeya kwenye milima na miteremko mikali kuhakikisha wanakagua magari yao kabla ya kuanza safari na wamiliki wa magari wasiruhusu magari yao kuendeshwa na madereva hao ili kuepusha ajali.
Imetolewa na:
BENJAMIN KUZAGA – ACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.