Na. Dennis Gondwe, KIKUYU KUSINI
ELIMU ndiyo mkombozi kwa vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kuwasaidia kutoa mchango katika maisha yao na maendeleo ya taifa la Tanzania.
Kauli hiyo ilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde alipokuwa akiongea na wanafunzi na walimu wa shule za sekondari katika hafla ya kugawa vifaa vya maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi tukio lililofanyika Shule ya Sekondari Wella iliyopo Kata ya Kikuyu Kusini.
Mavunde ambae pia ni Waziri wa Madini alisema “elimu ninaamini kwamba ndiyo mkombozi wa kweli kwa vijana wetu na elimu hii itawasaidia kwenda kuwafanya wakatoe mchango wao na kulitumikia taifa la Tanzania na wao pia katika maisha yao. Baada ya kubaini tunachangamoto katika maabara zetu nyingi za vifaa, nikasema nianze na awamu ya kwanza na hii haitakuwa mwisho nitajitahidi kuzifikia maabara nyingi zaidi. Leo nimeanza na shule tatu na mzigo wa kwanza huu umenigharimu shilingi 9,000,000 na nitaendelea kufanya hivi sababu dhamira yangu ni kuhakikisha wanafunzi wetu wanafanya vizuri”.
Akielezea mikakati yake kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema ni kukuza elimu. “Mkakati wa kwanza ambao ninao kwenye kukuza elimu katika Mkoa wa Dodoma na hasa Jimbo la Dodoma mjini. Nimesikia changamoto ya walimu wa sayansi hii ni changamoto kubwa na mimi suluisho ninalo na nimeshaanza kulifanyia kazi. Tuna shule za sekondari 43, lakini Dodoma umepita Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao una uwezo wa kutuunganisha kupitia teknolojia ya kisasa mwalimu mmoja wa sayansi mfano wa Shule ya Sekondari Msalato anaweza akawafundisha wanafunzi wote wa Dodoma kwa wakati huohuo. Tukipata seti 43 za televisheni zikafungwa shule zote, mimi kwa nafasi yangu nitakwenda kuongea na TCRA na watu wa Mfuko wa Mawasiliano na kampuni za simu niwaombe watuunganishie huu mkongo” alisema Mavunde.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo alisema kuwa halmashauri yake imepeleka shilingi 20,000,000 kukamilisha ujenzi wa maabara ya shule ya Sekondari Wella. “Mheshimiwa mbunge, hapa tayari unaona ujenzi unaendelea kwenye maabara yetu kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, sisi hatuwezi kukuangusha kwa sababu tunafanya kazi kwa kushirikiana tumeshaleta shilingi 20,000,000 hapa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara. Mheshimiwa waziri kwa maelekezo yako ya juzi ulituelekeza tutafute fedha na tumeshapata shilingi 8,000,000 kwa ajili ya kukamilisha matundu saba ya vyoo. Miongoni mwa changamoto ambazo zimezungumzwa na mkuu wa shule nimezipokea na nitakaa na timu yangu ya menejimenti na madiwani tuone namna bora ya kuzitatua” alisema Kayombo.
Aidha, alishukuru kwa vifaa vya maabara vilivyokabidhiwa na mbunge. “Mheshimiwa waziri, vifaa hivi ulivyotukabidhi leo ninakushukuru sana, ni miongoni mwa wabunge wachache wanaoyapenda majimbo yao. Mimi hii ni halmashauri yangu ya nne kama mkurugenzi, lakini nimekuwa nikikufuatilia sana kote nilipokuwa unapambana sana kuhakikisha jimbo lako linaenda vizuri, siyo kwenye elimu tu bali kwenye maeneo yote. Nikuombe moyo huu uendelee na sisi tupo bega kwa bega na wewe tutakupa ushirikiano wa kutosha na hakuna atakayekuangusha” alisema Kayombo.
Awali akiongelea mafanikio ya shule hiyo Mkuu wa Shule ya Sekondari Wella, Mwl. Adelifi Kaizirege alisema kuwa shule yake imefanikiwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi mwaka hadi mwaka. “Sambamba na hilo shule imefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga kidato cha tano na vyuo vya kati. Kufanya ukarabati wa vyumba vitatu vya madarasa kwa kuweka sakafu chini kupitia michango ya wazazi na wadau wa shule na kuongeza vyumba vitatu vya madarasa” alisema Kaizirege.
Kuhusu malezi na nidhamu ya wanafunzi alisema kuwa imeimarika sana. “Nidhamu ya wanafunzi imeimarika kutokana na juhudi ambazo uongozi wa shule kwa kushirikiana na walimu unazitumia na kuzisimamia. Wanafunzi wengi wanajitahidi kuwahi kufika shuleni kutokana na usimamizi wa walimu. Uongozi wa shule unawapongeza wazazi wote wanaotoa ushirikiano chanya katika kutatua changamoto za kinidhamu zinazowakabili watoto wao hasa utoro, kunyoa mitindo, kutoboa pua, kuvaa sketi fupi, kuvaa suruali zinazobana, kujihusisha kwenye mahusiano ya kimapenzi na ugomvi” alisema Kaizirege.
Jumla ya shule tatu za sekondari Wella, Makutopora na Mtemi Chiloloma zilipokea vifaa vya maabara za masomo ya sanyansi vyenye thamani ya shilingi 9,000,000.