Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumnza baada ya kufungua kongamano la biashara na uwekezaji Mkoa wa Ruvuma lililofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea
Baadhi ya wadau wa maendeleo kutoka mkoani Ruvuma walioshiriki kongamano la biashara na uwekezaji Mkoa wa Ruvuma lililofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea
Na Albano Midelo,Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amelitaja eneo lenye fursa nyingi za uwekezaji Ruvuma kuwa ni sekta ya kilimo.
Akizungumza wakati anafungua kongamano la Biashara na Uwekezaji la Mkoa kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea,Kanali Thomas ameyataja mazao makuu ya biashara yanayozalishwa kuwa ni ,kahawa,korosho na tumbaku.
Mazao ya chakula na biashara ameyataja kuwa ni mahindi,ufuta,soya,mbaazi,alizeti,mpunga,maharage,tangawizi na mzao mengine ya bustani.
“Mkoa wa Ruvuma ndiyo mzalishaji mkubwa wa kwanza wa mazao ya nafaka nchini,hata hivyo lengo la Mkoa ni kuzalisha zaidi hivyo tunahitaji uwekezaji kwenye viwanda vya mbolea na viuatilifu kwenye kilimo”,alisema RC Thomas.
Hata hivyo amesema Mkoa wa Ruvuma umetenga maeneo ya uwekezaji katika kilimo cha Pamoja yenye jumla ya hekta 25,017 ambazo zimetambuliwa na zinatakiwa kuwekezwa.
Amesisitiza kuwa Mkoa wa Ruvuma una mazao ya kutosha kuanzisha viwanda vya uchakataji ambapo kwa mwaka 2022/2022 Mkoa ulizalisha tani 25,284.5 za korosho,tani 13,700 za kahawa,tani 7,970.2 za ufuta,tani 5,152.3 za soya,tani 2,846.9 za mbaazi na tani 731,224 za mahindi.
Amesema katika msimu wa mwaka 2022/2023 Mkoa wa Ruvuma umezalishaji tani 1,598,163 za mazao ya chakula hali iliyosababisha Mkoa kuwa na ziada ya chakula tani 1,043,525.
Ameutaja Mkoa wa Ruvuma kuwa una mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na kwamba kuna jumla ya hekta 197,108.2 zonazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo hadi sasa ni hekta 7,388.3 tu zilizoendelezwa sawa na asilimia 3.7.